Meneja Mkazi wa AfDB nchini Tanzania, Bi. Patricia Laverley, akizungumza leo Aprili 29, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa tathmini ya athali za miladi ya kupunguza vifo vya wajawazito uliofadhiliwa na benki ya maendeleo ya Afrika (AfDB)
Dkt. Sunday Rwebangila, Daktari Bingwa Mwandamizi wa Magonjwa ya akina Mama na Uzazi na mwakilishi wa Wizara ya afya akizungumza leo Aprili 29, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa tathmini ya athali za miladi ya kupunguza vifo vya wajawazito uliofadhiliwa na benki ya maendeleo ya Afrika (AfDB).
Tathmini ya athari za Mradi wa Kupunguza Vifo vya Wajawazito unaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeonesha mafanikio makubwa katika uboreshaji wa huduma za afya ya uzazi Tanzania Bara na Zanzibar. Tathmini hiyo imebaini kuwa vifo vya wajawazito vimepungua kutoka 578 hadi 265 kwa kila watoto 100,000 waliozaliwa hai.
Akizungumza leo Aprili 29, 2025 jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari, Meneja Mkazi wa AfDB nchini Tanzania, Bi. Patricia Laverley, amesema kuwa mradi huo pia umesaidia kupunguza vifo vya watoto wachanga kutoka 90 hadi 50 kwa kila watoto 1,000 waliozaliwa hai.
Bi. Laverley ameeleza kuwa tathmini huru ya maendeleo ya Benki ya AfDB (IDEV) ilifanyika ili kutoa ushahidi wa msingi kuhusu athari za mradi wa SMMPR, kubainisha changamoto za utekelezaji na kutoa mapendekezo ya kuboresha utendaji wa mradi. Alisisitiza umuhimu wa mafunzo kwa watumishi wa afya ya uzazi ili kuendelea kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga.
Mradi huo umejikita katika kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya kama haki ya binadamu, pamoja na kuboresha miundombinu ya afya kwa mama na mtoto. Utekelezaji wake umehusisha ujenzi na ukarabati wa zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, taasisi za mafunzo, na nyumba za watumishi wa afya. Vituo vya afya vilivyochaguliwa pia vimepewa vyumba vipya kwa ajili ya huduma za mama na mtoto.
Aidha, mradi huo umechangia upatikanaji wa vifaa tiba, jenereta za dizeli, samani, magari ya wagonjwa, na huduma muhimu kama maji safi na umeme, ili kuhakikisha huduma zinatolewa ipasavyo.
Kwa upande wa maeneo yaliyolengwa, mradi umefanyika katika mikoa ya Tabora, Mara, na Mtwara kwa Tanzania Bara, pamoja na mikoa ya Kati, Kusini Unguja, Pemba Kusini, na Pemba Kaskazini kwa upande wa Zanzibar. Utekelezaji wake umegharimu dola za Kimarekani milioni 65.75, ambapo asilimia 90 ilitolewa na AfDB na asilimia 10 na Serikali ya Tanzania.
Kwa upande wake, Dkt. Sunday Rwebangila, Daktari Bingwa Mwandamizi wa Magonjwa ya akina Mama na Uzazi na mwakilishi wa Wizara ya afya, amesema kuwa Mradi wa Kupunguza Vifo vya Wajawazito unaofadhiliwa na AfDB ni hatua muhimu katika jitihada za kitaifa za kupambana na vifo vitokanavyo na uzazi. Ameeleza kuwa mradi huo umeendana na vipaumbele vya taifa, hasa katika kuimarisha afya ya Watanzania.
Dkt. Rwebangila amesema kuwa katika utekelezaji wa mradi huo, wataendelea kubaini changamoto zilizopo pamoja na maeneo yanayohitaji maboresho, huku wakitunza mafanikio yaliyopatikana kwa ajili ya maendeleo endelevu.
“Sisi kama watendaji tuna jukumu la kuunga mkono jitihada za serikali kumaliza kabisa vifo vya mama na mtoto. Tunapaswa kuhakikisha kuna sera, mipango na mikakati madhubuti – ya kitaifa na kimataifa – ambayo inaleta matokeo chanya,” amesema.
Ameongeza kuwa tangu kuanza kwa mradi huu, mafanikio yameanza kuonekana. Kwa mfano, ripoti ya takwimu ya mwaka 2023 imeonesha kuwa vifo vya wajawazito nchini vimepungua kutoka 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2005 hadi kufikia 104 mwaka 2022.
.jpeg)
Dkt. Rwebangila amesema kuwa matokeo hayo si tu yameleta matumaini kwa watekelezaji wa huduma za afya, bali pia yamewapa nafasi ya kutambuliwa kimataifa. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipokea Tuzo ya Kimataifa ya Uongozi kwa mchango wake wa kupunguza vifo vya mama na mtoto.
Baadhi ya wadau wakijadili tathmini ya athari za miradi ya kupunguza vifo vya wajawazito unaofadhiliwa na benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB)
Aidha, Dkt. Rwebangila amesisitiza kuwa haitakubalika mama yeyote kupoteza maisha wakati akijifungua. Ametoa wito wa juhudi za ziada hasa katika kupunguza vifo vya watoto wachanga, ambao bado wanakumbwa na changamoto kubwa ndani ya mwaka wao wa kwanza wa maisha.