Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Ridhwan Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa ORICA baada ya kutembelea banda lao katika maadhimisho ya Wiki ya Usalama na Afya Mahala Pa Kazi yanayendelea kufanyika mkoani Singida.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Ridhwan Kikwetev akitembela banda la Orica Tanzania na kujifunza kuhusu shughuli zao za ulipuaji migodi wakati akifanya ukaguzi katika maadhimisho ya Wiki ya kimataifa ya Usalama mahali pa kazi inayofanyika kitaifa mkoani Singida
WAKATI Dunia ikiadhimisha Siku ya Usalama Kazini Aprili 28, 2025 chini ya kaulimbiu ‘Nafasi ya Akili Mnemba na Teknolojia za Kidijitali katika Kuimarisha Usalama na Afya Mahala Pa Kazi, Orica Tanzania inayojishughulisha na utengenezaji Pamoja na uuzaji wa baruti kwa ajili ya ulipuaji migodini imetoa wito wa kuhakikisha usalama unazingatiwa wakati wa kazi ili kuepusha madhara yatokanayo na ajali za baruti.
Akizungumza katika Maonesho ya Wiki ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi Duniani yanayoendelea Kitaifa mkoani Singida, Mhandisi wa Baruti kutoka Orica Bw. Boaz Samwel amesema kuwa baruti ni kihatarishi kikubwa migodini na huweza kuleta madhara makubwa endapo hakitatumiwa kwa kuzingatia kanuni za matumizi sahihi.
“Kupitia maonesho haya, tumekuja na teknolojia ya kisasa inayotumia Akili Mnemba kwa ajili ya ulipuaji bila madhara yoyote na kupitia teknolojia hii, kazi ya ulipuaji inaweza kufanyika kwa ufanisi na usalama zaidi pasipo kuwepo mtu yeyote ndani ya eneo la karibu na mlipuko.” amesema Bw.Samwel.
“Tofauti na miaka ya nyuma, Teknolojia imebadili kwa kiasi kikubwa sana mfumo mzima wa ulipuaji na kuifanya kazi hii kuwa rahisi na salama zaidi, kipaumbele kikubwa kikiwa ni kulinda uhai wa watu, mazingira na ufanisi katika uzalishaji.
Amesema ili kupunguza na kuondoa madhara yanayoweza kutokea maeneo ya migodini, licha ya Orica kuwa watengenezaji na wauzaji wa baruti , wao pia wamekuwa wakitoa ushauri kwa matumizi sahihi ya teknolojia salama katika kazi hiyo kwa kuzingatia sheria na taratibu zote za Wakala wa Usalama na Afya Mahala Pa Kazi (OSHA).
Bw.Boaz amezitaja baadhi ya teknolojia zinazotumia akili Mnemba kuwa ni pamoja Blast IQ, ORBS, 4D, RHINO, OREpro 3D, ENVIROTrack, FRAGTrack na GroundProbe inayoweza kuhisi na kutambua mabadiliko yoyote katika mwamba na kutoa taarifa wakati huo huo na kuzuia ajali inayoweza kusababishwa na kuanguka kwa mwamba.
Amesema uwekezaji huu ni maendeleo makubwa katika sekta ya madini ikiendelea kubadilika kwa njia ya kidijitali na uvumbuzi.
Akitoa mtazamo mpana kuhusu dhamira ya Orica Tanzania, Daniel Paul, Mtaalamu wa Rasilimali Watu kwa Kanda ya Kusini mwa Afrika ya Orica — akizungumza kwa niaba ya Mhandisi Asha Mambo, Meneja wa Eneo la Orica Tanzania — alisema:
“Katika Orica Tanzania, tunaamini kuwa usalama, afya, na ustawi wa wafanyakazi ni nguzo kuu za mafanikio ya biashara yetu. Kama sehemu ya Orica Limited, kampuni inayoongoza duniani katika vilipuzi vya kibiashara, mifumo ya ulipuaji na huduma za madini inayofanya kazi katika zaidi ya nchi 100, tumejikita katika kuweka viwango vya juu zaidi vya usalama — katika shughuli zetu pamoja na katika sera na taratibu.
Alisisitiza zaidi kuwa usalama si jukumu la wachache, bali ni wajibu wa pamoja kwa wadau wote — imani ambayo inaendelea kuimarisha mafanikio na uimara wa Orica Tanzania.
Orica inafanya kazi katika zaidi ya nchi 100, ikiwa na zaidi ya miaka 150 ya uzoefu. Mashirika na makampuni mbalimbali yameshiriki katika maonesho hayo yaliyodumu kwa wiki nzima.
Akiongea wakati wa ufungaji, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Ridhiwani Kikwete amewataka washiriki kuimarisha juhudi za usalama wa wafanyakazi na kuwa kipaumbele katika shughuli zao.