Farida Mangube, Morogoro
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kimeendelea kufanya Ukarabati wa miundombinu na ujenzi wa majengo mapya kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), unaotekelezwa katika kampasi zote za chuo hicho hapa nchini.
Mtaalamu wa Ujenzi wa Mradi wa HEET kutoka SUA, Mhandisi Japhet Maduhu, alisema hayo wakati wa ziara ya kutembelea ili kuona maendeleo ya ujenzi na ukarabati wa majengo katika Kampasi ya Mizengo Pinda (Katavi), Kampasi ya Solomon Mahlangu Mazimbu na Kampasi ya Edward Moringe zilizopo Morogoro.
Mhandisi Maduhu alieleza kuwa lengo la mradi huo ni kufanikisha dhima ya kufufua na kupanua uwezo wa vyuo vikuu katika kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kukidhi mahitaji ya soko la ajira.
Alisema mradi unahusisha ujenzi wa majengo mapya tisa, yakiwemo majengo matatu ya maabara, hosteli mbili, na majengo manne kwa ajili ya shughuli za kitaaluma. Aidha, majengo 18 yanakarabatiwa ili yaendane na kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia, kwa kuweka mifumo mipya ya TEHAMA na umeme, badala ya miundombinu ya zamani iliyokuwepo.
“Kwa sasa, utekelezaji wa mradi umefikia zaidi ya asilimia 8. Wakandarasi wote wako kazini na wanaendelea na shughuli za ujenzi.
Kwa upande wa SUA, tumepata Shilingi bilioni 73.6, ambapo takribani Shilingi bilioni 58 zimeelekezwa kwenye shughuli za ujenzi kwa kampasi zote,” alisema Mhandisi Maduhu.
Alifafanua kuwa ukarabati wa majengo unatekelezwa kwa kipindi cha mwaka mmoja, ukianza Desemba 2024 na kutarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu. Ujenzi wa majengo mapya, ambao unatarajiwa kuchukua miezi 18, utahitimishwa Juni 2026.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Mradi wa Ujenzi wa Kampasi ya Solomon Mahlangu, Mhandisi Enock Kamagu, alisema ujenzi unaendelea vizuri licha ya changamoto ya mvua zinazoendelea kunyesha mkoani Morogoro.
Aliongeza kuwa awali mkandarasi alikumbwa na changamoto ya ucheleweshaji wa vifaa vya ujenzi, lakini kwa sasa hali imeimarika na wana imani kuwa kazi itakamilika kwa wakati.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko SUA, Bi. Suzana Magobeko, alisema kukamilika kwa mradi huo kutachochea ongezeko la udahili wa wanafunzi katika kampasi zote tatu za chuo hicho, pamoja na kupanua fursa zaidi za kuwafikia wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
Aidha, alisisitiza kuwa uboreshaji wa miundombinu ya kufundishia, kujifunzia na kufanya utafiti utaongeza ubora wa mafunzo, na kuwasaidia Wahadhiri na watafiti kufikia malengo yao.