WAFANYABIASHARA 50 waliyokuwa wamepanga kwenye fremu za jengo lililoporomoka Kariakoo Novemba 16, 2024 wamefungua kesi katika Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi wakidai fidia ya Sh. Bilioni 40 kwa wamiliki wa jengo.
Walalamikaji wanadai kiasi hicho cha pesa kama fidia ya hasara ya uwekezaji na biashara waliyowasababishia kutokana na uzembe wa wadaiwa kufanya ujenzi wa chini kwa chini kinyume na makubaliano ya mkataba wa upangaji kati yao uliosababisha kuporomoka kwa jengo hilo.
Katika hati ya madai iliyowasilishwa mahakamani hapo na wakili Peter Madelekaa, wadai hao wanadai kuwa, fidia hiyo inatokana na uzembe wa ujenzi wa chini kwa chini uliosababisha kuporomoka kwa jengo hilo na kuharibu fremu zao za rejareja na biashara za jumla.
Aidha, wameiomba Mahakama itamke wadaiwa Zenabu Ismail kama mwakilishi wa kisheria wa marehemu Abdallah Salim, Ashour Ashour,
kama mwakilishi wa marehemu Awadhi Ashur Abeid na Leondela Mdete kwamba walikiuka mikataba ya upangaji kati yao kwa kufanya ujenzi wa kizembe.
Hati hiyo ya madai inaelekeza kwamba kesi hiyo imefunguliwa na Kanali Naftal Swai na wenzake 49 ambao walikuwa wamepanga katika jengo lililopo Kiwanja namba 12, kitaru 7, eneo la Kariakoo, Manispaa ya Ilala, jijini Dar es Salaam.
Inadaiwa kati ya Januari 2023 hadi Desemba 31, 2024, wadai na wadaiwa waliingia katika mikataba ya upangaji kwa njia ya mdomo na kwa maandishi kuhusu jengo hilo.
Inadaiwa kuwa wadai waliwekeza na kuendesha biashara mbalimbali zikiwemo maduka ya rejareja, thamani ya jumla ya uwekezaji na biashara za zilizokuwa zikiendeshwa katika jengo ni Sh bilioni 40.
Pia, wadai wanadai kwamba wadaiwa walikiuka masharti na vigezo vya mkataba wa upangaji kati yao kwa walifanya ujenzi wa chini kwa chini kwa uzembe na bila idhini, ulisababisha kuporomoka kwa jengo hilo.
Hivyo, walalamikaji wanaomba Mahakama itoe hukumu na amri dhidi ya wadaiwa na pia wameomba mahakama itamke kwamba gharama za kesi zilipwe na wadaiwa.
Kesi hiyo ambayo imepangwa kusikilizwa mbele ya Jaji Mohamed Gwae, imetajwa leo Aprili 29,20255 mbele ya Naibu Msajili Rose Kangwa.