Na Mwandishi Wetu – Singida
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Ridhiwani Kikwete, amesisitiza umuhimu wa wananchi kujiunga na kuchangia Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ili kunufaika na mafao mbalimbali yakiwemo Mafao ya Matibabu kwa Wananchi waliojiajiri. Kwa upande wa wafanyakazi wa NSSF, Mhe.Waziri amewataka kuendelea kuhudumia wanachama kwa weledi.
Mhe. Ridhiwani amesisitiza hayo alipotembelea banda la NSSF kwenye Maonesho ya Wiki ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi Duniani, yanayofanyika Kitaifa katika viwanja vya Mandewe, mkoani Singida.
Amesema NSSF ina jukumu kubwa la kutoa huduma za hifadhi ya jamii kwa wanachama wa sekta binafsi na kuwafikia wananchi waliojiajiri kupitia Mfumo wake wa Hifadhi Skimu, ili kuhakikisha hata wale waliojiajiri wenyewe wanapata mafao ya muda mfupi na mrefu.
“NSSF ina wajibu mkubwa wa kuimarisha maisha ya wanachama wake, hasa pale wanapokumbwa na majanga yanayoathiri kipato chao. Hivyo amesisitiza kuendelea kutoa elimu ya mafao na huduma zinazotolewa na Mfuko huo kwa wananchi.
Aidha, Mhe. Ridhiwani alionesha kuridhishwa na jinsi NSSF ilivyotekeleza dhana ya usalama na afya mahala pa kazi.
Kwa upande wake, Meneja wa NSSF Mkoa wa Singida, Bw. Oscar Kalimilwa, amesema NSSF imeshiriki maonesho hayo kwa lengo la kutoa elimu kuhusu hifadhi ya jamii, kusajili wanachama wapya kutoka sekta binafsi pamoja na wale waliojiajiri wenyewe.
Bw. Kalimilwa alisisitiza kuwa maonesho hayo yamewapa nafasi ya kuwakumbusha waajiri wa sekta binafsi juu ya wajibu wao wa kuwasajili na kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa wakati.
“Ninatoa rai kwa waajiri kuhakikisha michango ya wafanyakazi wao inawasilishwa NSSF kwa wakati kwani hilo ni takwa la kisheria. Kufanya hivyo kutawahakikishia wanachama kulipwa mafao yao kwa wakati na kuondoa usumbufu usio wa lazima,” alisema.
Vilevile, aliwahamasisha wananchi waliojiajiri, wakiwemo bodaboda, mama lishe, wavuvi, wakulima, wachimbaji wadogo, wasusi, vinyozi, wasanii na wajasiriamali wengine, kujiunga na kuchangia katika NSSF kupitia Hifadhi Skimu.
Alibainisha kuwa mwanachama aliyejiajiri anapaswa kuchangia si chini ya shilingi 30,000/- kwa mwezi ili kupata mafao mbalimbali yakiwemo ya matibabu, na shilingi 52,200/- mwanachama atapata Mafao ya matibabu yeye na familia yake wakiwemo watoto wanne. Ameongeza kuwa michango hiyo inaweza kufanyika kidijitali kupitia simu za kiganjani ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa uharaka.