Na John Bukukuku
Dar es Salaam, Aprili 30, 2025
Jeshi la Polisi nchini limepokea msaada wa pikipiki 15 kutoka kwa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) kwa lengo la kusaidia katika shughuli za doria na misako mbalimbali ili kuimarisha usalama wa raia na mali zao.
Akizungumza wakati wa kupokea pikipiki hizo kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, CP Awadhi Juma Haji, alisema msaada huo utasaidia kuongeza ufanisi katika utendaji wa kazi za kila siku, hasa katika maeneo yenye changamoto ya miundombinu.
“Pikipiki hizi zitatumika kikamilifu kuhakikisha wananchi wanaendelea kufanya shughuli zao kwa amani na usalama. Jeshi la Polisi linaendelea kujipanga kuhakikisha linakuwa karibu zaidi na wananchi,” alisema CP Awadhi.
Kwa upande wake, Mwanasheria wa Mgodi wa GGM, David Nzaligo, alisema utoaji wa pikipiki hizo ni sehemu ya mchango wao kwa jamii na hatua ya kuimarisha ushirikiano kati yao na Jeshi la Polisi, ambao ni wadau muhimu katika kuhakikisha mazingira salama ya uwekezaji.
“Huu ni mwendelezo wa jitihada zetu kurudisha kwa jamii na kushirikiana na vyombo vya usalama. Tunaamini kuwa mazingira ya usalama ni msingi imara kwa maendeleo ya shughuli za kiuchumi,” alisema Nzaligo.