Na Dennis Gondwe, KIZOTA
AFISA Elimu Awali na Msingi Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwl. Prisca Myalla ameongoza zoezi la upandaji miti 100 katika Shule ya Msingi Mahungu kwa wadau waliozaliwa Mwezi Aprili kwa lengo kuwaandalia mazingira mazuri ya kujisomea wanafunzi shuleni hapo.
Alisema kuwa Shule ya Msingi Mahungu ni shule iliyojengwa kwa fedha za serikali kuu kupitia mradi wa Boost awamu ya pili Mwaka wa fedha 2024/2025.
Akiongelea zoezi la upandaji miti katika shule hiyo, alisema kuwa ni kuunga mkono juhudi za serikali chini ya kauli hamasishi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ya ‘Mti wangu, Birthday yangu’.
“Tupo hapa watumishi tuliojumuika kutoka taasisi mbalimbali ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuanzia walimu, wauguzi hadi maaskari. Sisi ni timu ya watumishi waliozaliwa Mwezi Aprili ‘Team Aprili’. Leo tutapanda miti kutekeleza maono ya mkuu wa mkoa kwamba ‘Mti wangu, Birthday yangu’. Kwa hiyo, tutapanda miti 100 katika eneo hili la shule ili kuendelea kukijanisha Dodoma yetu, dhamira yetu Dodoma iendelee kuwa ya kijani” alisema Mwl. Myalla.
Kwa upande wake Afisa Elimu Kata ya Kiwanja cha Ndege, Mwl. Prisca Mgalula alisema kuwa zoezi la upandaji miti ni ishara ya uwajibikaji kwa ‘Team April’.
“Leo ni siku ya pekee kwetu, tumependelea kuja kutembelea Shule ya Msingi Mahungu ikiwa shule mpya kabisa. Tunajua miti hii itaenda kuwasaidia watoto kuwa na mandhari nzuri ya kujifunzia, pia walimu watakuwa na mazingira mazuri ya kufundishia. Zoezi hili ni hamasa ya Afisa Elimu Awali na Msingi Jiji la Dodoma, Madam Prisca Myalla. Sisi wadau wa timu Aprili tutakuja kuitembelea miti tuliyopanda, kuona inaendelea kukua au la. Mkuu wa shule atasimamia hili” alisema Mwl. Mgalula.
Nae Mwalimu wa Taaluma Shule ya Msingi Mahungu, Mwl. Hadija Nasibu alisema kuwa miti inamchango katika kukuza taaluma na kuongeza ufaulu. “Sisi walimu wa Mahungu tumerufahishwa na zoezi hili na tumelipokea vizuri ikiwa ni ubunifu wa Afisa Elimu Awali na Msingi Jiji la Dodoma.
Tunamuahidi kuwa miti hii tutaitunza na tutaimwagilia na itakuwa vizuri, nae akija hapa atafurahia kuona maendeleo yake. Miti inawasaidia watoto kupata kivuli wakati wa kujisomea na kujadiliana na hatimae kupata matokea mazuri na kupandisha kiwango cha ufaulu” alisema Mwl. Nasibu.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mahungu, Mwl. Onesphory Massawe alisema kuwa shule hiyo ilikabidhiwa tarehe 22 Aprili, 2025.
“Tuna kila sababu ya kumshukuru Madam Prisca Myalla alihakikisha usiku na mchana halali kuhakikisha majengo haya yanakamilika na wanafunzi wanaanza masomo hapa. Leo tunaona amehamasisha ‘team April’ kutoka taasisi mbalimbali kupanda miti ya vivuli na matunda ambayo itawasiadia watoto kupata kivuli na matunda. Tunamshukuru sana Mungu aendelee kumbariki sana. Nasi tunaahidi kuitunza miti hii kwa sababu maji yapo ya kutosha, tumepiga marufuku kuleta mifugo hapa na tunashirikiana na kamati ya shule kuhakikisha miti hii inatunzwa” alisema Mwl. Massawe.
Shule ya Msingi Mahungu ilianza rasmi tarehe 22 Aprili, 2025 ikiwa na wanafunzi 331 waliohamishiwa kutoka shule mama ya msingi Sokoine na Kizota kwa lengo la kuwapunguzia wanafunzi kutembea umbali mrefu wa kilometa zaidi ya sita kufuata shule ilipo.