
Kampuni ya ASAS Group of Companies yenye makao yake makuu mkoani Iringa, Tanzania, imetangaza hatua ya kihistoria ya kuwaongezea madereva wake mshahara kwa zaidi ya asilimia 80 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Mei Mosi – Siku ya Wafanyakazi Duniani.
Kupitia taarifa yao rasmi, ASAS imesisitiza kuwa madereva wao si wafanyakazi tu bali ni mashujaa wa kweli wanaoendesha maisha ya kampuni hiyo, ambayo kwa zaidi ya miaka 80 imehudumia Watanzania kupitia sekta ya usafirishaji na bidhaa za maziwa.
“Kwa zaidi ya miaka 80, usafirishaji kwetu si biashara tu, ni maisha yetu. Siku hii ya Wafanyakazi tunawapa heshima ya kweli mashujaa wetu – Madereva wa malori – kwa kuwaongezea mishahara yao kwa zaidi ya asilimia 80,” imesema taarifa hiyo.
ASAS imeeleza kuwa uamuzi huo umeungwa mkono kikamilifu na Bodi ya Wakurugenzi wa kampuni hiyo na kuwa ni sehemu ya kutambua thamani ya kazi halisi isiyoonyeshwa kwa maneno pekee bali kwa vitendo.
Aidha, wameeleza shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuweka mazingira wezeshi ya kazi kwa wafanyakazi nchini.
“Hii si Mei Mosi ya sherehe tu, ni salamu ya heshima kwa roho ya kazi na wale wanaoibeba kwa moyo wa kweli,” imeeleza ASAS.