*************
Na Yusufu Kayanda
Afisa Uhusiano Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Sixmund Begashe, amesema heshima kubwa aliyoipata ya kutangazwa kuwa Mtumishi Hodari wa Wizara ya Maliasili na Utalii ni heshima kwa wanahabari wote nchini, pamoja na watumishi wote wa wizara hiyo kutokana na ushirikiano mzuri waliouonesha katika kuufahamisha umma kuhusu matokeo chanya ya utekelezaji wa kazi za wizara na taasisi zake.
Bw. Begashe amesema hayo leo mkoani Singida, mara baada ya kupokea salamu nyingi za pongezi kutoka kwa viongozi wa wizara hiyo, watumishi wenzake, waandishi na wahariri wa vyombo vya habari, pamoja na watu mbalimbali, kufuatia kutangazwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kuwa Mtumishi Hodari wa mwaka 2024/2025.
“Nimeungwa mkono na wanahabari wengi nchini katika kutekeleza majukumu yangu. Wamekuwa ni sehemu ya familia yangu kikazi. Tumeshirikiana vyema na watumishi wenzangu, viongozi katika ngazi mbalimbali, pamoja na familia yangu. Hali hiyo imenipa nafasi ya kufanya vizuri katika kuhabarisha umma kuhusu matokeo chanya ya utekelezaji wa kazi za wizara yetu. Hivyo, uhodari huu ni wetu sote,” alisema Bw. Begashe.
Aidha, ameongeza kuwa heshima hiyo inaendelea kumhamasisha kufanya kazi kwa bidii zaidi, huku akiendelea kushirikiana vyema na wanahabari wote chini ya miongozo bora ya msemaji wa wizara pamoja na viongozi wote kwa mujibu wa kanuni na taratibu za utumishi wa umma.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, pamoja na kuwapongeza watumishi wote wa wizara hiyo kwa kazi nzuri wanazozifanya, alimpongeza Bw. Begashe kwa kutangazwa Mtumishi Hodari na pia kuwatakia watumishi wote nchini Sikukuu Njema ya Mei Mosi.