Na: Calvin Gwabara – Morogoro.
Utafiti uliofanywa jijini Dar es
salaam na maeneo mengine ya dunia umeonesha kuwa kuwahusisha wanafunzi kwenye
shughuli mbalimbali na matukio ya kisayansi kunasaidia kuongeza uwezo wao wa
udadisi na kupenda masomo ya sayansi.
Kauli hiyo imetolewa na Profesa
mbobevu wa kemia kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Ndaki ya Sayansi
asili na Tumizi Prof. Faith Mabiki wakati akizungumza na wanafunzi wa Kidato cha
tano na sita katika shule ya sekondari ya ALFAGEMS iliyopo Manispaa ya Morogoro
Mkoani Morogoro katika mafunzo maalumu iliyoandaliwa na wananchama wa Pan
African Chemistry Network kwa lengo la kuwahamasisha kupenda masomo ya sayansi
hususani kemia.
“Tupo hapa leo kwakuwa tunaamini
katika utafiti huo kwamba tunahitaji kuwashirikisha watoto wetu kwenye matukio
ya kisayansi ili kukuza udadisi wao na hivyo kusaidia kuongeza idadi ya
wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi ambayo watu huamini kuwa ni magumu lakini
kupitia mafunzo ya aina hii kwa vitendo mara kwa mara na kuipenda kemia wanaweza
kuona kuwa masomo ya sayansi sio magumu kama inavyodhaniwa” Alieleza Prof.
Mabiki.
Prof. huyo wa Kemia kutoka Ndaki
ya Sayansi Asili na Tumizi (CoNAS) SUA amewataka kutambua kuwa nchi inahitaji
wakemia wengi ili kusaidia kufanya kazi kwenye viwanda mbalimbali ambavyo
Serikali inahamasisha wawekezaji kuja kujenga kwakuwa bila kufanya hivyo nafasi
hizo zitachukuliwa na wageni.
Amewataka wanafunzi hao na
wengine nchini kuona nafasi ya kemia kwenye maisha ya kila siku kwenye kila
eneo la maisha akitolea mfano wingi wa bidhaa zinazoongoza kwa kutumiwa
madukani zinazotengenezwa kupitia uchanganyaji wa kemikali mbalimbali na kupata
bidhaa pendwa kwa jamii ikiwemo vinywaji, hivyo mafunzo ya iana hiyo yatasaidia
kuzalisha idadi ya wanakemia wengi na kuchangia maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake mratibu wa
mafunzo hayo Mkemia Dkt. Frank Rwegoshora amesema kuwa mafunzo ya aina hiyo ni
muhimu sana kwa wanafunzi hao ambao wana mapenzi na masomo ya kemia na
ukizingatiwa kuwa ndio wanatarajia kwenda kusoma vyuo vikuu wanahitaji kujua
umuhimu na faida za kusoma kemia na fursa zilizopo duniani kupitia fani hiyo
muhimu.
Mratibu wa mafunzo hayo Mkemia Dkt. Frank Rwegoshora akizungumza malengo ya mafunzo hayo. |
“ Kwakweli tumefurahi sana sisi
kama waandaaji lakini pia walimu na zaidi wanafunzi 150 ambao wamejitokeza kwa
wingi na kufurahia mafunzo hayo yaliyofanyika kwa nadharia na vitendo yaliyotolewa
na walimu na wabobevu wa kemia kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine na tunaamini
tumezalisha jeshi la wataalamu wa kemia kupitia mafunzo haya” alieleza Dkt.
Rwegoshora.
Dkt. Rwegoshora amesema
wamefanikiwa kufikia wanafunzi wa shule hiyo leo lakini zipo shule nyingi
nchini ambazo zina wanafunzi wa aina hiyo na wengine wenye uwezo mkubwa na
mapenzi na kusoma kemia na kuwa wakemia, lakini wana woga na maneno ya baadhi
ya watu kuwa kemia ngumu hivyo wanahitaji kufikiwa na kupewa moyo na kuoneshwa
fursa zilizopo ikilinganishwa na masomo mengine.
“Tunatoa shukrani nyingi kwa
wafadhili wa mafunzo haya Pan African Chemistry Network na Royal Society of
Chemistry kwa msaada wao mkubwa katika kufanikisha hamasa hii muhimu kwa
wanafunzi wetu na wanasayansi wachanga ambao wameonesha kufurahi na kuahidi
kuchagua masomo ya kemia kwenye masomo yao ya ngazi za juu” alieleza Dkt.
Rwegoshora.
Wakieleza furaha yao mara baada
ya mafunzo hayo baadhi ya wanafunzi hao akiwemo Maganja Jeremiah amesema
wamefurahi kutembelewa na wataalamu hao lakini kubwa zaidi mafunzo hayo
yamewaonesha fursa kubwa zilizopo kwenye fani ya kemia pamoja na mchango wa
wataalamu wa kemia kwenye maendeleo ya Viwanda na uchumi wa Taifa.
“Tunawashukuru sana hakika
binafsi ninasoma mchepuo wa sayansi lakini nilikuwa na woga kuhusu swala la
maisha baada ya kuhitimu chuo kikuu fani ya kemia, lakini kwa maelezo na
ushahidi uliotolewa na wataalamu hawa kutoka SUA, sina woga tena na nitachagua
kusoma SUA fani hii ili niisaidie nchi yangu” alisema Maganja.
Nae mwanafunzi Prosper Rey
amesema kupitia mafunzo kwa vitendo wamejifunza vitu vingi ambavyo walikuwa
hawavifahamu na kuahidi kuendelea kuvitumia kwenye maisha yao na kila siku nyumbani
lakini pia kwenye masomo yao hasa wakati wa mitihani yao ya mwisho.
“Elimu hii itatuwezesha na sisi
kuwa mabalozi wazuri wa masomo ya kemia kwa wanafunzi wenzetu na kwa jamii
kuondoa woga uliosambaa miongoni mwa watu kuhusu ugumu wa masomo ya sayansi
hasa kemia ili jamii zaidi ielewe na kuhamasika kuisoma na kuitumia kwenye
maisha yao” Aalieleza Prosper.
Mafunzo hayo yametolewa walimu wa
Kemia na Fizikia kutoka chuo hicho Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kwa
ufadhili wa Pan African Chemistry Network na Royal Society of Chemistry.
MATUKIO KATIKA PICHA WAKATI WA MAFUNZO HAYO