Na mwandishi wetu
Benki ya NMB imedhihirisha tena nafasi yake kama Mwajiri Kinara nchini kwa kudhamini na kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), yaliyofanyika kitaifa mkoani Singida.
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na maelfu ya wafanyakazi kutoka sekta mbalimbali nchini, yakiwemo mashirika ya umma na binafsi, taasisi na vyama vya wafanyakazi, yakilenga kuenzi mchango wa wafanyakazi katika maendeleo ya taifa.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiambatana na viongozi waandamizi wa Serikali na wageni mbalimbali waalikwa.
Ujumbe wa NMB katika maadhimisho hayo umeongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo, Bi. Ruth Zaipuna, akiwa na baadhi ya viongozi wakuu na wafanyakazi wa benki hiyo walioungana na wenzao kuadhimisha siku hiyo muhimu.
Kupitia ushiriki wake, NMB imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kuwekeza katika ustawi wa rasilimali watu, kuboresha mazingira ya kazi na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha sekta ya ajira nchini.
Benki hiyo pia imewatakia wafanyakazi wote nchini maadhimisho mema ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, ikiwa ni sehemu ya kutambua na kuthamini mchango wao mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa taifa.