Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameendelea kuwa kielelezo cha uongozi bora kwa vitendo, akionyesha njia ya utendaji kazi wenye weledi, jambo ambalo linapaswa kuigwa na watumishi wengine wa umma.
Akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi), Kunenge amesema , Rais Samia amekuwa mstari wa mbele kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili wananchi.
Ameeleza, ni wajibu wa wafanyakazi wote nchini kufanya kazi kwa bidii ili kuondoa kero zinazowakabili wanajamii.
Aidha Kunenge ameeleza kuwa, kwa sasa mkoa umeanza mazungumzo na wawekezaji ili kuhakikisha wafanyakazi wanapatiwa mikataba ya ajira pamoja na kuchangia katika mifuko ya hifadhi ya jamii.
Awali, Mratibu wa TUCTA Mkoa wa Pwani, Susan Shesha, ametaja baadhi ya changamoto zinazowakabili wafanyakazi kuwa ni pamoja na mishahara midogo isiyoendana na hali halisi ya maisha, pamoja na baadhi ya waajiri kutotoa mikataba ya ajira, kuwazuia wafanyakazi kushiriki sherehe za Mei Mosi, na kushindwa kuchangia mifuko ya hifadhi ya jamii.
Katika hatua nyingine, Kunenge amezitaka taasisi zote kuwasilisha majibu ya changamoto zilizobainishwa ndani ya wiki moja.
Mtumishi wa kitengo cha habari ofisi ya mkuu wa mkoa wa Pwani ambae amepata tuzo ya mfanyakazi bora, Nasra Mondwe ameshukuru na kusema imempa morali wa kufanya kazi na kujituma kwa bidii.



