Wafanyakazi wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke wakionyesha mshikamano wao kwa kubeba bango wakati wa maandamano ya kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani, yaliyofanyika leo Mei 1, 2025 katika Viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe Jijini Dar es Salaam.
…….
Wafanyakazi wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke wameungana na wafanyakazi wote nchini kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani, huku wakitumia fursa hiyo muhimu kukumbushana wajibu wao wa kutoa huduma bora ya umeme kwa wananchi.
Akizungumza katika maadhimisho hayo yaliyofanyika leo Mei 1, 2025 jijini Dar es Salaam, Kaimu Meneja wa TANESCO Mkoa wa Temeke, Mhandisi David Mhando, amesema maadhimisho haya yamekuwa na maana kubwa kwao, kwani yamewapa nafasi ya kujitathmini na kuimarisha uwajibikaji kazini.
“Siku hii ni muhimu sana kwetu kama wafanyakazi. Ni muda wa kukumbushana kuhusu wajibu wetu wa kufanya kazi kwa bidii na kujituma kwa ajili ya kutoa huduma bora na ya uhakika kwa wananchi,” amesema Mhandisi Muhando.
Ameongeza kuwa wafanyakazi wa TANESCO wana jukumu kubwa la kuhakikisha miundombinu ya umeme inakuwa imara muda wote ili kuwezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika.
Aidha, amewataka wafanyakazi wa wilaya za Mbagala, Yombo na Kurasini kufanya kazi kwa weledi, ubunifu na kujitolea kwa ajili ya maendeleo ya taifa, kwani umeme ni injini ya uchumi.
Kwa upande wake, mfanyakazi wa Idara ya kutengeneza miundombinu ya Umeme wa TANESCO Mkoa wa Temeke,
Sadiki Mwakyusa, ameeleza kuwa katika maadhimisho ya mwaka huu, wamejivunia mafanikio makubwa waliyopata ikiwemo kupunguza tatizo la kukatika kwa umeme katika mkoa huo.
“Miundombinu ya umeme imeboreshwa kwa kiasi kikubwa, na wafanyakazi wanafanya kazi kwa bidii na moyo mkubwa, tunaamini kuwa upatikanaji wa umeme utaendelea kuimarika kadri siku zinavyosonga mbele,” amesema Mwakwisha.
Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani mwaka huu yamebeba kauli mbiu: “Uchaguzi Mkuu 2025 Utaleta Viongozi Wanaojali Haki na Maslahi ya Wafanyakazi, Sote Tushiriki.” ambapo yamefanyika Mkoa wa Dar es Salaam, huku Mgeni rasmi akiwa Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Albert Chalamila.