KONGAMANO la kwanza la kodi linatarajiwa kufanyika Mei 8, mwaka huu jijini Dar es Salaam litakalo wakutanisha watunga sera, wataalamu wa kodi, wafanyabiashara, na watafiti kwa lengo la kujadili mbinu za kupanua wigo wa kodi na kuimarisha ulipaji wa kodi wa hiari na kuongeza mapato ya nchi.
Kongamano hilo limeandaliwa na Chuo cha Kodi kwa ushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 2,2025, Mkuu wa Chuo cha Kodi, Profesa Isaya Jairo, amesema kongamano hilo ni jukwaa mahsusi la kujadili mikakati ya kuimarisha ulipaji wa kodi kwa hiari pamoja na njia za kuwahamasisha wajasiriamali walioko kwenye sekta isiyo rasmi kuingia katika mfumo rasmi wa ulipaji kodi.
“Kuna sekta zisizo rasmi kama wafanyabiashara wadogo, machinga na biashara za mtandaoni. Watu hawa wanafanya biashara lakini wengi hawalipi kodi. Kongamano hili litaangazia sheria na mbinu za kudhibiti ukwepaji wa kodi, kuzuia uingizaji wa bidhaa hafifu kutoka nje ya nchi, na kuhimiza matumizi ya teknolojia katika usimamizi wa kodi,” amesema Profesa Jairo.
Ameogeza kuwa kongamano hilo linafanyika wakati TRA ikiendelea na mageuzi ya kisheria na kiteknolojia kwa lengo la kuboresha mfumo wa kodi, huku changamoto ya sekta isiyo rasmi ambazo zinachangia takribani asilimia 45 ya pato la taifa zikiendelea kushughulikiwa.
Profesa Jairo ametoa wito kwa wananchi kushiriki kongamano hilo ili kutoa mchango wao utakaosaidia kutengeneza mapendekezo ya sera bora, kuimarisha ushirikiano na wadau, na kuchochea uhiari wa ulipaji kodi kwa maendeleo ya taifa.
Kaulimbiu ya kongamano ni “Kuongeza Wigo wa Kodi na Kuimarisha Ulipaji Kodi kwa Hiari Tanzania.” Washiriki watajadili mada kuu na mada ndogo mbili: Kupanua Wigo wa Kodi na Kurasimisha Sekta Zisizo Rasmi, pamoja na Kuzuia Ukwepaji wa Kodi.