*Rais Samia aipongeza REA utekelezaji miradi ya umeme vijijini
*Kiongozi wa Mwenge ahamasisha matumizi ya nishati safi na salama
Mufindi – Iringa
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ussi ameipongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa utekelezaji wa mradi wa umeme jazilizi (Densification 2C) unaotekelezwa kwa kiasi cha shilingi bilioni 17 Mufindi ili kukuza maendeleo yenye tija kwa wananchi.
Amebainisha hayo leo Mei 2, 2025 wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa ujazilizi 2C kwenye mbio za mwenge wa uhuru katika Wilaya ya Mufindi, Kitongoji cha Ilala mkoani Iringa.
Amesema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutawezesha matumizi ya nishati ya umeme ya kupikia na kuondoa adha ya akina mama na baba kutembea kwa umbali mrefu kutafuta sehemu ya kusaga mahindi.
Vile vile amesema kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha kwa REA kuwezesha utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini na kukuza uchumi wa wananchi.
“Rais Samia anawapongeza sana REA kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kuwaunganishia umeme wananchi hususan maeneo ya vijijini. Anawapongeza na kuwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii kwa manufaa ya watanzania,”. Amesema bw. Ussi.
Aidha, Msimamizi wa miradi ya REA kanda za nyanda za juu kusini, Mha. Danstan Kalugira amesema kuwa REA inaendelea kuhakikisha inafikisha umeme vijijini ili kuboresha huduma za wananchi kwa kuwapatia umeme wa uhakika Watanzania wote.
Kwa upande wake, meneja wa TANESCO wa wilaya ya Mafinga, Mha. Modest Mahururu amesema wilaya hiyo imeendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama katika shule za msingi na Sekondari na watu binafsi, taasisi za Serikali na zisizo za Serikali pamoja na vituo vya kutolea huduma za afya zenye kuhudumia watu zaidi ya 100.
Naye, mkandarasi anayetekeleza mradi huo kutoka Sagecom energy na Telecom Sas, Mha. Festo Samson, amesema mradi huo umefikia asilimia 52 na usimamishaji wa nguzo za umeme umekamilika katika vitongoji 81 kati ya 101 ambapo wanatarajia kuukamilisha kabla ya mwezi Oktoba mwaka huu.