Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, ametoa wito kwa watendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, wakiwemo Afisa Ardhi, Mwanasheria na Madiwani, kushirikiana kwa karibu katika kutatua migogoro ya ardhi kwenye kata zote za wilaya hiyo.
Akizungumza wakati wa kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani wilayani Same, Mhe. Kasilda alisema Serikali imeweka mkazo mkubwa katika kuhakikisha migogoro ya ardhi inatatuliwa kwa haraka ili kuwawezesha wananchi kuendelea na shughuli za uzalishaji bila vikwazo.
“Watendaji wote wa Halmashauri, akiwemo Afisa Ardhi, Wanasheria na watendaji waliopo kwenye kata, wanapaswa kushirikiana na Madiwani kufika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kusikiliza na kutatua changamoto zinazohusiana na ardhi. Haya ni maelekezo mahsusi kutoka kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe. Mohammed Mchengerwa,” alisema DC Kasilda.
Aidha, aliwapongeza madiwani kwa kusimamia vyema ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri kwa kushirikiana na watendaji, hatua aliyoeleza kuwa inaongeza kasi ya maendeleo katika wilaya.
Katika kikao hicho, Baraza la Madiwani wa Wilaya ya Same limeidhinisha kwa kauli moja kupandisha madaraja watumishi 230 wa kada mbalimbali ndani ya Halmashauri hiyo. Uamuzi huo umetajwa kuwa sehemu ya mkakati wa kuongeza morali na ufanisi kazini.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, Yusto Mapande, alisema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha haki na stahiki za watumishi zinalindwa kwa kuzingatia uwajibikaji na utendaji wa mtu mmoja mmoja.
“Tumekuwa tukipima utendaji wa kila mtumishi kwa kuzingatia vigezo halali. Watumishi waliopandishwa madaraja wamekidhi masharti hayo, na tutaendelea kuhakikisha tunatoa motisha kwa wanaojituma kwa bidii kazini,” alisema Mapande.
Ameongeza kuwa Halmashauri itaendelea kufanya tathmini ya mara kwa mara kwa watumishi wake ili kuhakikisha ufanisi unabaki kuwa kigezo kikuu cha maendeleo ya taasisi hiyo, huku akisisitiza umuhimu wa maadili na nidhamu kazini.