MSAJILI wa Vyama vya Siasa Tanzania, Jaji Fransis Mutungi amewataka wananchi wawe makini na matumizi ya akili bandia au akili unde (AI), na habari za uongo ambazo zinalenga kusambaza propaganda na kupotosha umma.
Jaji Mutungi ameyasema hayo Mei 3, 2025 jijini Dar es Salaam katika kikao maalumu na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari kujadili masuala tofauti ikiwemo maandalizi ya Uchaguzi Mkuu.
“Ni vyema tukawa makini kipindi hiki hususan viongozi wa vyama vya siasa, tudumishe amani na mshikano kwani ndiyo msingi wa maendeleo, tuepuke na habari ambazo hatuna uhakika nazo hasa wakati huu katika matumizi ya teknolojia”Amesema
Hata hivyo amewataka viongozi wa vyama vya siasa kuwahimiza wananchi wakiwemo wanachama wao, kufuata sheria kudumisha amani na mshikamo hususan kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Pamoja na hayo amesema wanaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa uchaguzi ikiwemo Tume Huru ya Uchaguzi na ile ya Zanzibar, kuhakikisha wanazingatia maadili na kudumisha amani kufanikisha uchaguzi huru, haki na amani.