Na Mwandishi wetu, Kiteto
MBUNGE wa jimbo la Kiteto Mkoani Manyara, Edward Ole Lekaita amewatoa hofu wakazi wa eneo hilo juu ya ujenzi wa barabara za kiwango cha lami zilizoahidiwa kujengwa na Serikali.
Ole Lekaita amesema anapenda kutoa taarifa za ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara za Kongwa- Kiteto – Simanjiro- Arusha) na Handeni- Kibirashi- Kijungu – Kibaya – Njoro – Chemba – Singida.
“Nafahamu kuwa sote tunajua umuhimu wa ujenzi wa barabara hizi mbili kwa uchumi wa Kiteto kwa ujenzi wa kiiwango cha lami, amesema Ole Lekaita.
Amesema ujenzi wa barabara hizo mbili kwa kiwango cha lami imekuwa kilio cha muda mrefu sana kwa wananchi wote wa Kiteto.
“Mnafahamu pia kuwa nimepaza sauti mara nyingi sana bungeni kuelezea umuhimu wa ujenzi kiwango cha lami kwa barabara hizi mbili,” amesema Ole Lekaita.
“Ndugu wananchi wenzangu mtakumbuka kuwa mnao tarehe 16. 6. 2023 tuliweza kusaini mikataba ya barabara saba nchini zijengwe kwa kiwango cha lami kwa kupitia mfumo mpya wa EPC + F ambao ni mfumo unaotumika anchi zingine duniani ambapo mkandarasi anajenga baarabara mwenyewe kwa pesa zake na kulipwa na serikali baadae na polepole baada ya ujenzi kukamilika,” amesema.
Ameeleza kuwa utaratibu huo ndiyo ulipelekea serikali kukubali kusaini mikataba hiyo tangu mwaka 2023 na barabara tajwa hapo juu zilikuwepo katika barabara saba zilizopitishwa na Bunge.
“Mtakumbuka pia wakandarasi walifika Kiteto na tulifanya mkutano mkubwa Engusero kuhusu mradi huu wa ujenzi wa barabara hizi mbili,” amesema Ole Lekaita.
Ameeleza kuwa baada ya majadiliano zaidi kati ya serikali na mkandarasi ikagundulika kuwa mkandarasi hakuweza kuendelea na ujenzi wa barabara hizo kutokana na sababu mbalimbali za kiufundi.
“Mtakumbuka pia kuwa Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan alieza baadhi ya sababu za kiufundi kwenye miradi ya EPC + F kwa umma,” amesema Ole Lekaita.
Amesema kutokana na changamoto hizo za kiufundi na wakati majadiliano bado yanaendelea kati ya wakandarasi na Serikali kuhusu mpango EPC + F – Serikali imepanga mpango wa kutenga pesa za ndani za bajeti kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hizo mbili kwa awamu.
“Barabara Handeni – Kibirashi- Kijungu – Kibaya – Njoro- Chemba – Singida 460KM itaanza kujengwa kilometa 50 KM kutoka Handeni kuja Kibaya na Kilometa 50 KM kutoka Kibaya kwenda Kisima,” amesema Ole Lekaita.
Amesema barabara Kongwa- Kiteto – Simanjiro- Arusha KM 453 itaanza kujengwa kwa kilometa 70 kuanzia Arusha na taarifa rasmi zitatolewa na Wizara kwa barua na atawajulisha siku siyo nyingi.
“Kusema la moyoni kwangu kama Mbunge wenu ningetamani sana Barabara ya Kongwa – Kiteto – Simanjiro- Arusha Ujenzi wa Kilometa 70 uanze kujengwa kuanzia Kibaya kwenda Kongwa ( ushawishi na mazungumzo bado unaendelea) lakini pia ni ukweli kuwa kila mbunge angependa ujenzi wa barabara hii uazie kwake.
“Vilevile, ziara ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye ziara ya Tanga alisisitiza kuwa ujenzi wa barabara Handeni – Kibirashi- Kijungu – Kibaya – Njoro ijengwe kwa ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi na hii ni ishara tu kuwa Serikali inatambua umuhimu wa Ujenzi wa Barabara zetu hizi,” amesema.
“Kwa dhati kabisa tunamshukuru qMhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kubuni mbinu na mikakati ya kutafuta fedha kwaajili.ya Ujenzi wa barabara hizi zetu mbili ambazo ni muhimu sana kwa uchumi wa jimbo letu,” amesema.
“Tuendelee kumwombea Mhe. Rais afya njema na Mungu amwezeshe kupata maono makubwa kwa ajili ya kutafuta fedha kwa ajili ya barabara hizi zetu mbili, asante kwa kunisikiliza na Mungu awabariki, Kiteto ya maendeleo,” amesema.