Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya Nyasa Mkoani Ruvuma,wakifuatilia taarifa mbalimbali kwenye kikao cha robo ya tatu kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri hiyo.
Baadhi ya Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya Nyasa Mkoani Ruvuma,wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya hiyo Peres Magiri(hayupo Pichani)wakati akitoa salamu za Serikali kwenye Barza la Madiwani jana.
Picha no694 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Nyasa Mkoani Ruvuma Khalid Khalif,akizungumza kwenye kikao cha robo ya tatu cha Baraza la Madiwani katika Ukumbi wa Halmashauri,kulia kwake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Nyasa.
………………..
Mkuu wa Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, Peres Magiri, amewataka Madiwani wa Halmashauri hiyo kushirikiana na watendaji wa vijiji na kata waliopo kwenye maeneo yao kubuni vyanzo vipya vya mapato pamoja na kuboresha vile vilivyopo, ili kuiwezesha Halmashauri kujitegemea na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Magiri aliyasema hayo jana, wakati akitoa salamu za Serikali kwenye kikao cha robo ya tatu cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri na kuhudhuriwa na wakuu wa idara, watendaji wa kata na Madiwani.
“Halmashauri ikiwa na vyanzo vingi zaidi vya mapato itakuwa na uwezo wa kukusanya fedha nyingi na kutoa huduma bora za kijamii kwa wananchi, ikiwemo huduma za afya, elimu na mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na walemavu,” alisema Magiri.
Aliongeza kuwa ukusanyaji wa mapato lazima uendane na nidhamu ya matumizi ya fedha, na Madiwani wahakikishe wanasimamia ipasavyo mapato yanayopatikana kupitia vyanzo mbalimbali.
“Madiwani kupitia kamati zenu hakikisheni mnafuatilia na kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili mjiridhishe kama inalingana na fedha zilizotolewa na Serikali, badala ya kuwa watazamaji,” alisisitiza.
Aidha, aliwataka watumishi wapya kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kujenga imani kwa wananchi, na kujiepusha na tabia zisizoendana na maadili ya utumishi wa umma kama kuzalisha migogoro na chuki baina ya Serikali na wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Khalid Khalif, alisema kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Halmashauri imepangiwa kukusanya Shilingi bilioni 2.4, sawa na ongezeko la asilimia 66 kutoka bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024.
Alisema hadi kufikia Machi 30, 2025, Halmashauri ilikuwa imekusanya Shilingi bilioni 1.8, sawa na asilimia 78.36, na hadi Aprili 28, 2025, walikuwa wamekusanya zaidi ya asilimia 82 ya mapato ya ndani yaliyokusudiwa kwa mwaka huo wa fedha.
Kwa mwaka wa fedha 2025/2026 unaoanza Juni 30, 2025, Halmashauri hiyo imepangiwa kukusanya Shilingi bilioni 3.2, ikiwa ni ongezeko la asilimia 35 kutoka bajeti ya sasa.
Khalif alieleza kuwa ili kufanikisha lengo hilo, Halmashauri imeweka mikakati mbalimbali ya kuongeza mapato na kudhibiti upotevu, ikiwemo kuweka mazingira bora kwa wawekezaji kuchimba makaa ya mawe, kununua leseni 20 kwa ajili ya uchimbaji huo, pamoja na kutenga Shilingi milioni 20 kwa ajili ya biashara ya makaa ya mawe yanayopatikana kwa wingi wilayani humo.
Mbunge wa Jimbo la Nyasa, Stella Manyanya, alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitano (2020–2025), ushirikiano kati ya watumishi na uongozi umewezesha kuvuka malengo ya mapato ya ndani na kupata hati safi.
Naye Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Zefania Manyeshi, aliipongeza Halmashauri ya Nyasa kwa kupata hati safi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa miaka mitatu mfululizo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa, Stewart Nombo, aliwasisitiza Madiwani kwenda kuwaeleza wananchi mambo mazuri yaliyofanywa na Serikali katika kipindi cha miaka mitano ili yaeleweke kwa wananchi waliowachagua.