Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam. Kampuni maarufu ya michezo ya kubashiri, betPawa, imesaini mkataba wa mwaka mmoja a wenye thamani ya Sh 639,466,554 kwa Ligi ya Mpira wa Kikapu (BDL) ya mkoa wa Dar es Salaam.
Huu ni udhamini wa kwanza na wa kihistoria katika mpira wa kikapu hapa nchini usainiwa jana ambapo mkuu wa Maendeleo ya Michezo na CSR wa betPawa Raquel Puig pamoja na Katibu mkuu wa BD, Mpoki Mwakipake katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Don Bosco, Upanga jana.
Akizungumza katika hafla hiyo, Puig alisema kuwa wanajisikia fahari kubwa kuchangua maendeleo ya michezo nchini, hasa mpira wa kikapu ambao ni moja ya michezo pendwa duniani.
“betPawa ipo mstari wa mbele kusaidia jamii ikiwa pamoja na michezo. Mpira wa kikapu ni moja ya michezo ambayo inawavutia na yenye mashabiki wengi.
Tunaamini kupitia udhamini huu, tutafikia lengo na kuchangia maendeleo ya michezo nchini.. Tumefanya hivyo katika nchi mbalimbali za ukanda wa Afrika Mashariki na Tanzania hii ni mara yetu ya pili kusaidia mchezo wa mpira wa kikapu,” alisema Puig.
Katika udhamini huo, wachezaji 12 na viongozi wanne kwa timu ambazo zitaibuka washindi katika mechi kwa upande wa wanawake na waume watazawadiwa fedha taslim Sh88, 750 kupitia Locker Room Bonus.
Fedha hizo zitalipwa moja kwa moja kwenye akaunti zao za simu kwa mujibu wa Meneja Masoko wa Afrika Mashariki wa betPawa wa Borah Ndanyungu.
“Ushirikiano huu ni mabadiliko makubwa kwa mpira wa kikapu wa Tanzania. Locker Room Bonus haitainua tu kiwango cha ushindani bali pia itatoa msaada wa kifedha ambao ni muhimu sana kwa wanamichezo wetu. Tunasubiri kwa hamu kuona jinsi hii itakavyobadilisha ligi,” alisema Ndanyungu.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa BD, Mpoki Mwakipake alisema kuwa udhamini huo umewapa faraja kubwa sana na kuwataka mashabiki wa mpira wa kikapu kutarajia ushindani mkubwa katika ligi ya mkoa ambayo imepangwa kuanza Juni 12.
“Udhamini huu ni wa kihistoria na utaleta hamasa kubwa kwa wachezaji ili kupata ushindi na kupata fedha. Zamani, wachezaji walikuwa wanashiriki mpira wa kikapu kama sehemu kujifurahisha, lakini sasa kupitia Locker Room Bonus, ushindani utakuwa mkubwa sana na hivyo kuchangia maendeleo kwa wachezaji,” alisema Mwakipake.
Wasanii wakitumbuiza wakati wa wakati wa hafla ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja wenye thamani ya Shh639, 466,554 kwa ajili ya udhamini wa ligi ya mpira wa kikapu ya mkoa wa Dar es Salaam (BDL).