Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde akimkabidhi tuzo ya Mwandishi Mahiri wa Habari za Madini ,Dotto Dosca Kwilasa Mwandishi wa Malunde Media (Malunde 1 blog) wakati wa hafla ya tuzo za Samia Kalamu Awards 2025.
TAZAMA VIDEO
Mwandishi wa habari na mtengenezaji hodari wa maudhui ya kidijitali kupitia Malunde Media (Malunde 1 Blog), Dotto Dosca Kwilasa, ameandika historia kwa kushinda tuzo ya Mwandishi Mahiri wa Habari za Madini katika tuzo kubwa za Samia Kalamu Awards 2025!
Tuzo hizo zilizotolewa katika hafla iliyofanyika Mei 5, 2025, katika ukumbi wa Super Dome Jijini Dar es salaam zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wanahabari, na wadau wa maendeleo, huku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa mgeni rasmi.
Katika hafla hiyo iliyopambwa kwa shamrashamra na heshima ya juu, Dotto Dosca Kwilasa ametambuliwa kwa kazi yake bora na yenye mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta ya madini nchini Tanzania.
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amemkabidhi Dotto Dosca Kwilasa, zawadi ya shilingi Milioni tano, cheti, madini ya Rubi pamoja na Leseni ya Utafiti wa Madini yenye ukubwa wa kilomita za mraba 20.
Dotto Kwilasa ambaye ni mwandishi wa habari, mtengenezaji na mchapishaji maarufu wa maudhui Mtandaoni ametambulika kwa uchambuzi wake makini, weledi wa hali ya juu, na matumizi bora ya teknolojia ya habari kuibua na kufikisha habari zenye tija kwa jamii.
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Dotto Dosca Kwilasa amesema:
“Ninatoa shukrani za dhati kwa waandaaji wa tuzo hizi, Malunde Media kwa kunipa jukwaa, na jamii kwa kuendelea kuunga mkono kazi zetu. Ushindi huu si wangu peke yangu, ni wa tasnia nzima ya habari ambayo inaendelea kuchangia maendeleo ya taifa letu.”
Malunde Media inayomiliki mtandao wa Malunde 1 blog, chini ya uongozi wa Kadama Malunde ambaye ni mwandishi wa habari mahiri akitokea mkoani Shinyanga, inaendelea kung’ara katika uandishi wa habari za maendeleo, huku ikitoa nafasi kwa waandishi wachanga na mahiri kama Dotto Kwilasa kung’ara katika ulingo wa habari kitaifa na kimataifa!
Tuzo za Samia Kalamu Awards zimeanzishwa kwa lengo la kutambua mchango wa waandishi wa habari nchini Tanzania katika kuhamasisha maendeleo kupitia kalamu zao, zikilenga sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, madini, mazingira, na utawala bora.
Dotto Dosca Kwilasa sasa anabaki kuwa kielelezo cha uandishi wa kisasa unaogusa jamii, unaoibua fursa na kuhamasisha maendeleo ya kweli kupitia kalamu yenye uzito na dhamira ya dhati.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwahutubia Viongozi, Wadau wa habari pamoja na wageni mbalimbali waliohudhuria hafla ya utoaji wa Tuzo za Samia Kalamu Awards 2025 kwa Waandishi wa Habari katika ukumbi wa The Super Dome Masaki Jijini Dar es Salaam tarehe 05 Mei, 2025.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akitoa hotuba katika hafla ya utoaji Tuzo za Uandishi wa Habari #SamiaKalamuAwards Tarehe 05 Mei, 2025 iliyofanyika katika ukumbi wa The Super Dome Masaki.
Katika hafla hiyo, Mhe. Rais amekabidhi tuzo mbalimbali kwa vyombo vya habari mahiri, wanahabari mahiri na chipukizi wa tasnia hiyo.
TCRA imeshiriki katika kuandaa hafla hiyo ikishirikiana na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA).