Waziri ya Katiba na Sheria Dkt Damas Ndumbaro amesema kuwa katika uongozi wa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan sekta ya Haki imeshuhudia jinsi inavyotekelezwa kwa vitendo.
Dkt Ndumbaro amezungumza hayo leo Mei 5, 2025 Mkoani Morogoro katika ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo maafisa sheria wa jeshi la magereza kuhusu huduma za msaada wa kisheria, Mapokezi ya wafungwa Magerezani na Adhabu mbadala.
Amesema sekta ya utoaji haki inajivunia Rais Samia kwakuwa mstari wa mbele kutekeleza haki kwa makundi mbalimbali ikiwemo wafungwa na mahabusu.
“Tumshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Sisi katika sekta ya Sheria, katika kipindi chake tumeona neno haki likitendewa haki, tumeona haki ikitamalaki katika kona zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunakumbuka aliunda tume ya haki jinai ambayo kitendo hiki kimeonesha kwanza ni mpenda haki na anataka wananchi wake wapate haki” amesisitiza Dkt. Ndumbaro
Aidha Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Eliakim Maswi amewasihi washiriki hao kutoa ushirikiano ili mafunzo hayo yawe na tija iliyokusudiwa
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt. Maduhu Kazi amesema kuwa Wizara hiyo kupitia Jeshi la Magereza imeendelea kuboresha urekebu Magerezani ili kuwezesha utoaji haki katika maeneo hayo.
Nae Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza CGP Jeremiah Katungu amesema kuwa mafunzo hayo yatasaidia kwa kiasi kikubwa kongeza ujuzi na mbinu za utekelezaji wa majukumu ikiwemo eneo la utoaji wa ushauri wa kisheria.
Jumla ya wataalamu wa sheria 120 wanashiriki mafunzo hayo ya siku tano ambapo mada mbalimbali zitawasilishwa ikiwemo Adhabu Mbadala, Mashauri ya kinidhamu, Mahakama Mtandao na Mabadiliko ya Sheria.