ILI kuwapa ujuzi utakaowasaidia kuongeza kipato na kujikwamua kiuchumi Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza nchini kimezindua programu ya mafunzo ya ujasiriamali na Stadi za Biashara kwa wafungwa nchini.
Akifungua programu hiyo leo Mei 06, 2025 katika gereza kuu Arusha, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza CGP Jeremiah Katungu ameipongeza IAA kwa kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha eneo la urekebishaji ambalo ndiyo jukumu kubwa la jeshi la magereza.
“Kasi ya IAA tumeiona, tangu tuliposaini makubaliano Septemba 2024 matokeo tunayaona, na sisi tunakwenda kwa kasi hiyo hiyo kuhakikisha kwamba tunayafikia tuliyokubaliana kwa maslahi mapana ya taifa letu; programu hii ni mwanzo mzuri na tutahakikisha tunawafikia wafungwa wengi zaidi,” amesema CGP Katungu.
CGP Katungu ameongeza kuwa pamoja na mafunzo hayo kwa wafungwa, zaidi ya maafisa na askari 100 wa jeshi la magereza wamedahiliwa kwa mwaka wa masomo 2024/2025 kwa ngazi ya shahada ya uzamili, ikiwa ni sehemu ya makubaliano kuwajengea uwezo waweze kutimiza majukumu yao kwa weledi na ufanisi.
Mkuu wa Chuo IAA Prof. Eliamani Sedoyeka amesema wajibu wao kama chuo ni kutoa mafunzo kwa ngazi mbalimbali na mafunzo haya kwa wafungwa ni mwanzo tu, huku akibainisha kuwa malengo yao kutoa mafunzo ya muda mrefu kuanzia ngazi ya cheti mpaka shahada ya uzamili kwa wafungwa.
Prof. Sedoyeka ameongeza kuwa katika kozi za muda mfupi IAA imeanza na programu hii ya ujasiriamali na wanatarajia kutanua wigo wa mfunzo kwa kuanzisha kozi nyingine ikiwepo udereva, ili wafungwa wanapomaliza vifungo vyao wawe na ujuzi, maarifa na kuwa vielelezo bora kwa jamii zao.
Naye Mkuu wa Kitivo Cha Utawala na Usalama IAA Dkt. Adonijah Abayo amesema Programu ya Mafunzo ya Ujasiriamali na Stadi za Biashara kwa wafungwa imeanza na wanafunzi 40 na yatatolewa kwa wiki mbili kwa kuanza na Gereza la Arusha na baadaye maeneo mengine, ambapo itawasaidia wafungwa wanaporudi mtaani kwenda kujiajiri na kukuza uchumi wao na uchumi wa nchi.