Mkuu wa mkoa wa Songwe Daniel Chongolo akizungumza wakati wa kufungua kikao cha siku tano cha Kamati ya pamoja ya wataalamu wa Tanzania na Zambia kujadili uimarishaji mpaka wa kimataifa baina ya nchi hizo kilichofanyika tarehe 5 Mei 2025 Tunduma, Songwe. Kushoto ni Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Hamdouny Mansoor na katikati ni Mkuu wa wilaya ya Momba Elias Mwandobo.
……………
Na Munir Shemweta, WANMM SONGWE
Kikao cha Kamati ya pamoja cha wataalamu wa Tanzania na Zambia kimeanza mkoani Songwe nchini Tanzania kujadili mpango kazi wa uimarishaji mpaka wa kimataifa baina ya nchi hizo.
Kikao hicho kimeanza tarehe 5 Mei 2025 na kutaratarajiwa kumalizika Mei 9, 2025 katika mji wa Tunduma mkoani Songwe na kuhusisha wataalamu kutoka nchi za Tanzania na Zambia.
Akifungua kikao hicho cha siku tano, Mkuu wa mkoa wa Songwe Daniel Chongolo amesema, Tanzania imejipanga kikamilifu kutekeleza zoezi la uimarishaji mpaka wa kimataifa kwa ajili ya ustawi wa nchi hizo mbili.
“Uimarishaji mpaka wa kimataifa kati ya Tanzania na Zambia una lengo la kuweka usimamizi mzuri wa mpaka baina ya nchi hizo pamoja na Kukuza amani, upendo, usalama na maisha ya watu wake”. Amesema Chongolo.
“Ni imani yangu kila mshiriki katika kikao hiki atatumia muda kuhakikisha uimarishaji mpaka wa kimataifa baina ya nchi zetu unakuwa na matokeo mazuri kwa ustawi wa nchi na wananchi wetu” amesema.
Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye ni kiongozi wa timu ya Tanzania kwenye kikao hicho Bw. Hamdouny Mansoor amesema, mkutano huo ni utekelezaji wa mpango wa Umoja wa Afrika kuhusu uimarishaji wa mipaka ya kimataifa kwa nchi za Afrika kufikia mwaka 2027.
” Ni nia ya Umoja wa Afrika kuzifanya nchi za Afrika kuwa na amani pasipo migongano wakati wa zoezi zima za uimarishaji mipaka ya kimataifa” amesema Mansoor .
Mpaka wa Tanzania na Zambia una urefu wa takriban km 345 ambapo km 100 ni nchi kavu, km 189 ni mto Kalambo na km 56 ziwa Tanganyika
Zoezi la uimarishaji mipaka ya kimataifa ni utekelezaji wa makubaliano ya Umoja wa Afrika kuwa, ifikapo mwaka 2027 mipaka baina ya nchi za Afrika iwe imeimarishwa.
Tanzania imepakana na nchi 10 ambazo ni Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, DRC, Zambia, Malawi, Msumbiji, Comoro na Shelisheli huku mipaka baina ya nchi hizo ikiwa imegawanyika katika sehemu mbili za nchi kavu na majini.
Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye ni kiongozi wa timu ya Tanzania kwenye kikao hicho Bw. Hamdouny Mansoor akitoa maelezo mafupi katika kikao cha kujadili uimarishaji mpaka wa kimataifa kati ya Tanzania na Zambia mkoani Songwe. Kulia ni Mkuu wa wilaya ya Momba Elias Mwandobo.
Ujumbe wa wataalamu kutoka Zambia ukiwa katika kikao cha Kamati ya pamoja ya wataalamu wa Tanzania na Zambia kujadili mpango kazi wa uimarishaji mpaka wa kimataifa baina ya nchi hizo.
Ujumbe wa Tanzania katika kikao Kamati ya pamoja ya wataalamu wa Tanzania na Zambia wakijadili uimarishaji mpaka wa kimataifa baina ya nchi hizo.
Timu ya wataalamu kutoka Tanzania na Zambia ikiwa katika kikao cha kujadili uimarishaji mpaka wa kimataifa wa nchi hizo tarehe 5 Mei 2025 katika mji wa Tunduma mkoa wa Songwe.
Picha ya pamoja ya mgeni Rasmi Dainiel Chongolo (Aliyekaa kati kati) na timu ya wataalamu wa kamati ya pamoja kutoka Tanzania na Zambia wanaokutana katika mji wa Tunduma mkoa wa Songwe kujadili uimarishaji mpaka wa kimataifa wa nchi hizo. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)