SERIKALI ya Tanzania imetangaza mageuzi makubwa ya sekta ya ardhi yanayolenga kuboresha usimamizi, kuchochea ukuaji wa uchumi, na kulinda haki za wananchi wake.
Akizungumza katika siku ya pili Mkutano wa Kimataifa wa Sekta ya Ardhi ulioandaliwa na Benki ya Dunia katika Makao Makuu ya Benki hiyo Jijini Washington DC, Marekani Mei 06, 2025, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Deogratius Ndejembi amesema mageuzi hayo yamefanywa na Serikali kupitia Sera ya Taifa ya Ardhi ya Mwaka 1995 (Toleo la Mwaka 2023) ambayo ilizinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Machi 17, 2025 jijini Dodoma.
Waziri Ndejembi amesema Sera hiyo inalenga kuboresha usimamizi wa ardhi kwa kuweka msingi imara wa haki, usawa na matumizi endelevu ya rasilimali hiyo muhimu.
‘‘Mageuzi haya yanatokana na uhitaji unaoendana na mahitaji ya sasa ya kijamii na kiuchumi, pamoja na kukabiliana na changamoto kama migogoro ya ardhi, ukuaji wa mijini na mabadiliko ya tabianchi,” amesema Mhe. Ndejembi.
Amesema miongoni mwa maboresho makubwa katika sera hiyo ni kuimarisha usalama wa milki za ardhi ya kilimo na ufugaji, kuweka uwazi katika taratibu za utwaaji wa ardhi na ulipaji wa fidia, pamoja na kuanzisha Tume ya Ardhi itakayoratibu utoaji huduma ili kuongeza ufanisi, uadilifu na uwajibikaji wa watumishi wa ardhi.
Aidha, sera inasisitiza matumizi ya teknolojia ambapo mfumo wa e-Ardhi utasaidia wananchi kupata huduma za ardhi mtandaoni, kufuatilia mwenendo wa maombi yao, na kuhakikisha uhakika wa kumbukumbu. Mfumo huo unalenga kupunguza urasimu na kuongeza uwazi katika utoaji wa hati miliki na usajili wa miamala ya ardhi.
Katika kuimarisha matumizi ya ardhi, sera imeweka mkazo katika upangaji bora wa matumizi ya ardhi mijini na vijijini, utunzaji wa maeneo nyeti, na kuhakikisha rasilimali ardhi inatumika kwa tija kwa ajili ya uwekezaji. Hii ni pamoja na kuimarisha mfumo wa upimaji, ramani na taarifa za kijiografia unaosaidia kuwa na maamuzi sahihi ya mipango ya maendeleo.
Sera imeweka msukumo mkubwa katika kuhakikisha usawa wa kijinsia kwa kutambua haki za wanawake kumiliki na kurithi ardhi pamoja na kushirikishwa kikamilifu katika maamuzi ya matumizi ya ardhi katika familia na jamii.
Katika mkutano huo, Tanzania ilipongezwa kwa hatua madhubuti ilizochukua kuhakikisha usalama wa umiliki wa ardhi kwa raia wake, ikiwa ni sehemu ya kutekeleza Lengo la Maendeleo Endelevu (SDG) 1.4.2, linalolenga kuhakikisha watu wote wakiwemo wazee, wanawake, vijana na jamii za asili, wanapata haki ya kumiliki na kutumia ardhi kwa usalama.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo umeongozwa na Mhe Ndejembi ambaye ameongozana na wataalamu kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na wataalamu kutola Ofisi ya Rais-TAMISEMI.