FARIDA MANGUBE, MOROGORO
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)limesitisha matumizi ya jengo la mwekezaji Sameer Ismail maarufu Lotto baada ya mbia hiyo kutofuata mashariti ya mkataba.
NHC imechukua hatua hiyo ya kusimamisha jengo hilo la ghorofa sita lililopo Kiwanja Na. 67/I, lililopo barabara ya zamani ya Dar es Salaam mjini Morogoro, baada ya kucheleweshwa kukamilika kwa miaka 17 tangu kuanzishwa ujenzi wake.
Meneja uhusiano na mawasiliano wa NHC Muungano Saguya akizungumza na waandishi wa habari alisema Mkataba huo ulisainiwa mwaka 2007 kwa lengo la kujenga jengo la kisasa kwa manufaa ya wakazi wa Morogoro.
“Mbia huyo alishindwa kufuata taratibu za ujenzi, ikiwa ni pamoja na kutotumia wataalamu waliothibitishwa, kutopata vibali halali, na kushindwa kuzingatia viwango vya usalama vya ujenzi,”alisema Saguya.
Aidha uamuzi huo umetokana na kushindwa kwa mbia, kampuni ya M/S Saze & Samo Investment Ltd, kukamilisha mradi huo pamoja na ukiukwaji mkubwa wa masharti ya mkataba wa ubia.
Saguya alisema licha ya kupewa maelekezo na onyo mara kadhaa, mbia huyo aliendelea na ujenzi kinyume na ushauri wa kitaalamu ambapo Septemba 27,2023, NHC iliamua kurejesha rasmi udhibiti wa mradi huo na kuweka ulinzi katika eneo hilo ili kulinda usalama wa wananchi.
“Baada ya kuingia mkataba na mbia huyu Shirika lilitarajia jengo hilo litakuwa limekamilika ndani ya miaka miwili ili liwe chachu ya kuleta Maendeleo ya kiuchumi katika Manispaa ya Morogoro lakini kwa muda mrefu mbia huyu amekuwa akisuasua kutekeleza mradi huo wa ujenzi wa gorofa sita kwa kuzingatia taratibu za ujenzi,”alisema.
Mbia aliendelea kukaidi maagizo ya Shirika, ikiwemo kuondoa wapangaji waliopo kwenye jengo ambalo halijakamilika wala kuidhinishwa kwa matumizi, hivyo kuhatarisha maisha ya watu na kukiuka mkataba wa ubia.
Alisema kuwa hatua ya kutwaa usimamizi wa jengo inalenga kuhakikisha jengo linakamilika kwa ubora unaokubalika, kwa kutumia wataalamu wa Shirika.
Pia alisema shirika litaangalia uwekezaji uliofanywa na mbia na kuchukua hatua stahiki za fidia kulingana na makubaliano ya kimkataba na sheria.
Kwa mujibu wa tathmini ya kiufundi iliyofanywa na Kitengo cha Ushauri wa Ujenzi cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (BICO) ilibaini kasoro kubwa zilizohatarisha usalama wa jengo hilo ambapo BICO ilishauri ujenzi usiendelee zaidi ya ghorofa ya tatu, lakini mbia aliendelea na ujenzi bila kibali kutoka Manispaa ya Morogoro wala NHC.
Wapangaji waliokuwa wakitumia jengo hilo wameiomba Serikali kupitia Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuhakikisha maboresho ya jengo hilo yanafanyika kwa haraka ili waweze kurejea kuendelea na shughuli zao za kiuchumi.
Emil Mshana Katibu wa wapangaji katika jengo hilo, alisema kuwa hatua ya kulifunga jengo imewaathiri kwa kiwango kikubwa kwani wengi wao wanaendesha biashara kwa mikopo na sasa wamekosa sehemu ya kufanyia shughuli zao.
“Leo tunatoa vitu vyetu kwenye maduka lakini hatujui tunavipeleka wapi. Kikubwa zaidi ni kwamba tumepoteza wateja wetu waliotuzoea kwa miaka 16 kuwa tupo ndani ya jengo la Lottos. Leo hii wanapokuja kututafuta hawatupati, hali hii inatuumiza sana,” alisema Mshana kwa masikitiko.
Mshana alisisitiza umuhimu wa kuheshimu mikataba ya ubia na ushirikiano, akitoa wito kwa pande zote kuhakikisha wanafuata taratibu zilizowekwa kisheria ili kuepuka athari kama walizozipata wao wapangaji.
Mpangaji Jane Lucas alisema walivyofika asubuhi kwa ajili ya kufungua biashara yake alishangazwa kukuta jengo limezungushwa bati na baadae alianza kuondoa vifaa vyake na hajui pa kuvipeleka,.
“Hapa kuna watu Wana mikopo na tegemeo ni hizi biashara, sijapendezwa na jambo hili ilitakiwa wake watuelezw na kutupa hata siku kadha, Sasa hapa tunaenda wapi,”alisema.
Sera mpya ya ubia ya NHC iliyozinduliwa Novemba 2022, Shirika hilo linaendelea kuimarisha usimamizi wa miradi na kuhakikisha utekelezaji wenye ufanisi na tayari miradi saba imekamilishwa na wabia, minne imerejeshwa kwa NHC, na wabia sita wamepewa notisi kwa kuvunja masharti ya mkataba.
NHC imewataka wabia wote kuwa waadilifu na kuwajibika katika utekelezaji wa miradi, huku ikiwasihi wananchi kushiriki kikamilifu katika miradi ya maendeleo kwa kuzingatia sheria, viwango na usalama.