![]() |
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi Kitaifa ya Maadhimisho ya Juma la Elimu (GAWE) 2025, Bw. Greyson Mgoi akizungumza kwenye moja ya mikutano ya washiriki wa Maadhimisho ya Juma la Elimu (GAWE) 2025. |
![]() |
Vikundi vya burudani vya wanafunzi vikitumbuiza kwa washiriki wa Maadhimisho ya Juma la Elimu (GAWE) 2025, ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Juma la Elimu (GAWE) 2025. |
WANACHAMA wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), wamefanya ziara katika shule mbalimbali ndani ya Halmashauri ya Mpimbwe, mkoani Katavi, ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Juma la Elimu (GAWE) 2025, yanayofanyika kitaifa mkoani Katavi.
Miongoni mwa shule zilizotembelewa na Washiriki wa Juma la Elimu, ni pamoja na Shule ya Sekondari Mirumba, Shule ya Msingi Ikuba na Shule ya Sekondari Chamalendi.
Akizungumza katika mikutano na wazazi, walimu, viongozi na wadau wengine wa elimu, Mratibu Taifa wa TEN/MET, Bi. Martha Makala aliwaomba wanajamii kupinga vikali mila na desturi ambazo zimekuwa kikwazo cha maendeleo ya elimu katika maeneo hayo ikiwemo, utaratibu potofu ujulikanao kama ‘Chagulaga’.
Amesema utaratibu huo umekuwa kikwazo cha mafanikio ya ndoto za elimu, hasa kwa wasichana maeneo hayo kwani huchangia kukatiza masomo kwa wasichana wengi. Ameitaka jamii kukemea vikali kwa utaratibu huo, kwani ni kikwazo cha maendeleo na mafanikio ya elimu kwa jamii hiyo.
“Kama wewe ni mwana ume na umefikia kuona nenda kaowe mkubwa mwenzako na si wanafunzi…kwa hili tunapenda kuhamasisha jamii, wazazi, viongozi wa Kata, wanafunzi na walimu kuungana pamoja tushirikiane na Serikali kupambana nalo,” alisisitiza Mratibu Taifa wa TEN/MET, Bi. Makala.
Washiriki hao wa juma la elimu, walipata fursa ya kuhamasisha Jamii kushirikiana na Serikali katika kutatua changamoto za elimu maeneo yao, ili kuchochea maendeleo ya sekta hiyo muhimu nchini.
Aidha walitembelea na kuangalia hali ya uandikishaji wa Elimu awali na Darasa la kujifunzia, katika Shule ya Msingi Ikuba iliyopo katika Halmashauri ya Mpimbwe mradi uliochochea uandikishaji wa wanafunzi wa awali kwa kiasi kikubwa katika eneo hilo.
Maadhimisho ya Juma la Elimu (GAWE) 2025, yanafanyika kitaifa mkoani Katavi, halmashauri ya Mpimbwe huku kaulimbiu ikiwa ni “Elimu Ujuzi kwa Maendeleo ya Taifa.” [Education for Skills Development and Socio-economic transformation], na kuratibiwa na Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET).