Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Stanslaus Nyongo akifungua Kongamano la Kwanza la Kodi lililoandaliwa na Chuo cha Kodi (ITA) lililofanyika leo Mei 8, 2025 jijini Dar es Salaam.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Yusuph Mwenda akiwa katika Kongamano la Kwanza la Kodi lililoandaliwa na Chuo cha Kodi (ITA) lililofanyika leo Mei 8, 2025 jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Chuo cha Kodi, Profesa Isaya Jairo akizungumza na waandishi wa habari akiwa katika Kongamano la Kwanza la Kodi lililoandaliwa na Chuo hicho.
…..
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Stanslaus Nyongo, amewataka Watanzania kutoa ushirikiano kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kutoa taarifa za ukwepaji wa kodi pamoja na kubuni mbinu bora zitakazosaidia katika ukusanyaji wa mapato kwa ufanisi.
Akizungumza leo Mei 8, 2025 Jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kwanza la Kodi lililoandaliwa na Chuo cha Kodi (ITA), Mhe. Nyongo amesema kuwa muda umefika kwa jamii nzima kutoa mawazo bunifu yatakayoboresha mfumo wa ulipaji wa kodi, na kuongeza makusanyo ya serikali.
“TRA imezindua tuzo mbili: moja kwa ajili ya mtoa taarifa za kodi na nyingine kwa mawazo bunifu kuhusu mbinu za kuongeza mapato. Mtoa taarifa anaweza kupata zawadi ya kati ya Shilingi milioni moja hadi milioni ishirini,” amesema Mhe. Nyongo.
Amepongeza Chuo cha Kodi kwa kuandaa jukwaa hilo ambalo lina lengo la kujadili mbinu rafiki za kuongeza wigo wa kodi na kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari bila shuruti.
Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, amesema kuwa kongamano hilo ni fursa muhimu kwa mamlaka kusikiliza maoni ya wadau na kutambua maeneo yanayohitaji maboresho, ili kuongeza wigo na ufanisi wa ukusanyaji wa kodi.
Naye Mkuu wa Chuo cha Kodi, Profesa Isaya Jairo, amesema kongamano hilo limewakutanisha wadau mbalimbali kujadili mada muhimu na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuongeza mapato ya serikali.
“Kupitia majadiliano haya, tunaamini tutaongeza wigo wa walipa kodi, kwani bado kuna changamoto ya watu kutojali au kutoelewa wajibu wao wa kulipa kodi stahiki,” amesema Prof. Jairo.
Kongamano hilo limebeba kaulimbiu isemayo “Kuongeza Wigo wa Kodi na Kuimarisha Ulipaji wa Kodi kwa Hiari” na limeambatana na uzinduzi wa motisha ya mtoa taarifa za kikodi pamoja na tuzo kwa mawazo bunifu ya ukusanyaji kodi.