DALALI mmoja anayeishi Kipunguni jijini Dar es Salaam, Charles Shirima amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashitaka 42 ikiwemo utakatishaji fedha kiasi cha Sh milioni mbili.
Mshitakiwa amesomewa mashtaka yake na wakili wa serikali Michael Shindai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Romuli Mbuya Aprili 6,2025
Shidai amedai kuwa mashtaka ya kwanza hadi ya tisa ni kuchapisha taarifa za uongo.
Inadaiwa kuwa kati Desemba 30,2024 maeneo yasiyojulikana,ndani ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania mshtakiwa alichapisha taarifa za uongo katika mtandao wa kijamii wa Facebook kuwa TULIA TRUST FOUNDATION inatoa mkopo hadi milioni 50,000,000 huku akijua sikweli
Aliendelea kudai kuwa mashtaka ya 10 hadi 17 ni kujifanya mtu mwingine na kujitambulisha kwa watu mbalimbali.
Inadaiwa kuwa katika tarehe tofauti kati ya Desemba 31,2024 hadi Aprili 2025 ndani ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania mshitakiwa huyo akijitambulisha kwa David Sylvester Mugasa, Upendo Lawrence Kiwelu na wengine 6 kuwa yeye ni Spika wa Bunge Tulia Acksob Mwansasu
Wakili Shidai aliendelea kudai kuwa mashtaka 18 mpaka 37 nikujipatia fedha kwa njia ya udanyanyifu kutoka kwa watu mbalimbali ambapo inadaiwa kati ya Januari 31,2025 mshtakiwa huyo alijipatia kiasi cha Sh milioni mbili kupitia namba mbalimbali zilizosajiliwa majina ya watu tofauti tofauti zaidi ya 20 akidai kuwa angeawapatia mkopo huku akijua kuwa siyo kweli.
Katika mashtaka kuanzia 38 mpaka 41 mshtakiwa anakabiliwa na tuhuma za kutumia laini iliyosajiliwa kwa majina ya mtu mwingine bila ruhusa ya mtoa huduma.
Inadaiwa, kati April 29,2025 maeneo ya Kipunguni B Wilaya ya Ilala Mkoa wa Dar es salaam mshtakiwa alitumia namba za simu zilosajiliwa kwa watu wengine huku akijua kufaya hivyo ni kosa kisheria.
Katika shtaka la 42 la utakatishaji fedha, mshtakiwa anadaiwa kati ya Desemba 24,2024 hadi Aprili 2025 alijipatia kiasi cha Sh milioni 2, 827,000 huku akijua fedha hizo ni mazalia ya kosa tangulizi la kujipatia fedha kwa njia ya udanyanyifu.
Hata hivyo mshtakiwa hakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa kosa la utakatishaji fedha halina dhamana. Kwa mujibu wa upande wa Mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado unaendelea.
Kesi hiyo itatajwa tena Mei 22,Mwaka huu saa 4:00 asubuhi kwa njia ya mtandao mshitakiwa akiwa mahabusu Keko.