FARIDA MANGUBE, MOROGORO
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe, amevitaka vyuo vikuu nchini kuhakikisha vinaandaa wanafunzi kuwa wabunifu na kuendana na kasi ya ukuaji wa teknolojia na mapinduzi ya viwanda, ili waweze kujiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa baada ya kuhitimu.
Akizungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe wakati akifungua kambi ya wajasiriamali iliyoandaliwa na chuo hicho, Mhe. Kigahe alisema ni wakati sahihi kwa vijana kuchangamkia fursa zinazotolewa na serikali kupitia taasisi zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara, kwa kutumia bunifu na ujuzi walionao kujikwamua kiuchumi.
Aidha amepongeza juhudi za Chuo Kikuu Mzumbe kwa kuwaandaa wanafunzi katika ujasiriamali, alisema chuo hicho kimevunja dhana ya awali kuwa kinalenga zaidi kuwaandaa viongozi, na badala yake sasa kinakuza wabunifu na wajasiriamali ikiwa ni moja ya mbinu ya kuwafanya wanafunzi wakitoka mzumbe waweze kujiajiri wenyewe.
“Baada ya kuona bunifu ya jokofu lisilotumia umeme bali mkaa, nimeona wazi kuwa vijana hawa wakipata mazingira mazuri wanaweza kuleta mageuzi makubwa katika jamii. Serikali kupitia halmashauri zake ifikirie kuwekeza kwenye bunifu kama hizi,” alisema Kigahe.
Aidha, aliwataka vijana kutumia vyema biashara mtandao kwa kubuni programu zitakazosaidia wafanyabiashara na wanunuzi kulinda uaminifu na kukuza masoko ya bidhaa zao ndani nan je ya nchi.
Kwa upande wake, Naibu Makam Mkuu wa chuo Taalama tafiti na ushauri elekezi Prof. Hawa Tundui akizungumza kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. William Mwegoha , alisema kambi hiyo hufanyika kila mwaka ikiwa na lengo la kuwapa wanafunzi uzoefu wa vitendo na kuwaandaa kwa maisha ya kujitegemea baada ya masomo.
“Tunataka vijana wanapohitimu wawe na ujuzi wa kutatua changamoto katika jamii hususan katika sekta za kilimo, maji na matumizi ya teknolojia kama akili bandia (AI),” alisema Prof. Tundui.
Kambi hiyo ya siku tatu kuanzia Mei 7 hadi 9, imewakutanisha wanafunzi, wahitimu, wafanyakazi wa chuo, makampuni mbalimbali na wadau wa maendeleo ambapo zaidi ya mawazo 10 ya biashara yaliwasilishwa, huku washindi wa tatu bora wakipata zawadi za fedha — mshindi wa kwanza Sh milioni 1, wa pili Sh 700,000 na wa tatu Sh 500,000.
Kambi hiyo imekuwa jukwaa la kukuza ubunifu, kuunganisha vijana na wadau wa maendeleo, na kuwasaidia kupata mrejesho wa kibiashara kutoka kwa wataalamu. Pia inawajengea uwezo wa kuanza miradi yao binafsi hata kabla ya kuhitimu.