Na: Mwandishi Wetu, Dar.
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetoa majina ya wanufaika wa mikopo ya elimu kwa ngazi ya Stashahada (Diploma) walioomba kwenye dirisha la mwezi Machi, 2025.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk. Bill Kiwia, kupitia Taarifa yake kwa Umma, Mei 05, 2025, ameeleza kuwa fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 1.94 zimetengwa ili ziwanufaishe wanafunzi 873.
Sambamba na hilo, taarifa hiyo imeeleza kuwa Bilioni 1.51 zimetengwa kwa ajili ya chakula na malazi, Milioni 408 kwa ajili ya ada ya mafunzo huku vitabu na viandikwa vikigharimu shilingi 16,700,000.
Aidha, ili kuona majina ya waliopata mikopo hiyo, waombaji wameelekezwa kuangalia taarifa zao kupitia akaunti walizoombea mikopo (SIPA).
Huu ni mwendelezo wa utekelezaji wa maamuzi yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuongeza wigo wa wanufaika wa mikopo kwa ngazi ya Stashahada, ambapo hadi sasa idadi ya wanufaika wa mikopo hiyo imeongezeka kutoka 2,700 mwaka 2024 hadi 6,644 mwaka 2025 ambao wanasoma fani mbalimbali za kipaumbele katika Taifa letu.