Katika juhudi za kuandaa mazingira bora ya elimu kwa kizazi cha teknolojia, Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) imechukua hatua muhimu kwa kusaini hati ya makubaliano ya ushirikiano na taasisi ya Tanzania AI Community, ili kuanzisha matumizi ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence – AI) katika ufundishaji na ujifunzaji kwa shule zote nchini.
Makubaliano hayo, yaliyosainiwa jana jijini Dar es Salaam, yanatarajiwa kudumu kwa kipindi cha miaka mitatu, yakiwa na lengo la kufanikisha mageuzi ya elimu kwa kutumia teknolojia bunifu inayoweza kumwezesha mwalimu kufundisha kwa ufanisi zaidi na kumpa mwanafunzi fursa ya kujifunza kwa njia za kisasa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dkt. Aneth Komba, alisema ushirikiano huo utawezesha walimu na wakuza mitaala kufundishwa jinsi ya kutumia AI kwa ufanisi. Alibainisha kuwa jukumu la TET litakuwa ni kutoa karikulum, silabasi na vitabu kwa wadau wa teknolojia ili kuhakikisha matumizi ya AI yanaendana na viwango vya elimu vilivyopo.
“Ni mapinduzi makubwa. AI itampunguzia mzigo mwalimu, na kwa kupitia teknolojia hiyo, kutakuwa na uwezo wa kutengeneza maswali ya ubunifu yatakayopima uelewa wa kina kwa wanafunzi,” alisema Dkt. Aneth.
Aliongeza kuwa teknolojia hiyo si tu kwamba itarahisisha kazi ya mwalimu, bali pia itaimarisha ubora wa elimu kwa kuandaa wanafunzi kwa dunia ya kisasa ya kisayansi na kiteknolojia. Alisisitiza kuwa TET iko tayari kufanikisha utekelezaji wa mpango huo na baada ya miaka mitatu, tathmini ya mafanikio itafanyika ili kujua maeneo yaliyohitaji maboresho.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tanzania AI Community, Essa Mohamedal, alisema lengo lao ni kuwawezesha walimu kutumia zana za AI kufundisha kwa tija zaidi na kuongeza ubunifu darasani.
“Tuko hapa kuwasaidia walimu wa Tanzania kutumia teknolojia ya AI ili kuleta mapinduzi ya kweli kwenye sekta ya elimu. Ushirikiano huu na TET ni hatua ya kihistoria,” alisema Mohamedal.
Makubaliano haya yanajiri wakati ambapo dunia nzima inashuhudia ongezeko la matumizi ya AI katika sekta mbalimbali, na Tanzania inaonekana kuchukua hatua za makusudi kujiweka katika nafasi ya kunufaika na teknolojia hiyo, hasa kwa kizazi kinacholelewa leo kwa ajili ya kesho ya kidigitali.