Na Silivia Amandius
Kagera.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa, amewasilisha mpango maalum wa kuongeza uzalishaji wa kahawa kutoka tani 60,000 hadi tani 200,000 ifikapo mwaka 2030, kwa kuwashirikisha kikamilifu vijana na wanawake.
Akizungumza katika kikao cha wadau wa kahawa mkoani humo, Mwassa alisema zaidi ya shilingi bilioni 250 zimepatikana kupitia zao la kahawa msimu wa 2024/2025, huku halmashauri zikivuna mapato ya ndani ya shilingi bilioni 7. Ili kuimarisha uzalishaji, mkoa umetenga hekta 10,000 kwa vijana na wanawake, zikiwemo hekta 2,000 kwa kila moja ya wilaya za Karagwe na Muleba.
Aidha, shamba la mfano limeanzishwa Kijiji cha Makongora, Muleba, ambapo vijana na wanawake 300 wamepewa ekari moja kila mmoja kwa uzalishaji wa kahawa. Serikali pia imeongeza bei ya kahawa kutoka shilingi 1,200 hadi 5,000 kwa kilo, na kutoa matrekta matano kusaidia maandalizi ya mashamba.
Mwassa alielekeza asilimia 20 ya mapato ya kahawa zirudi kusaidia sekta hiyo na akapiga marufuku uvunaji wa kahawa mbichi. Meneja wa Bodi ya Kahawa Kagera, Edmond Zani, alisema soko la kahawa aina ya Robusta limeimarika kimataifa, ingawa bado jitihada zaidi zinahitajika baada ya kukusanywa tani 54.2 tu kati ya lengo la tani 74.8 msimu huu.
Bodi ya Kahawa inashirikiana na TACRI kugawa miche 17,164,000 bure kwa wakulima, huku changamoto zikiendelea kuwa pamoja na kahawa hewa, utoroshaji kabla ya mnada, na matumizi hafifu ya kahawa ndani ya nchi. Wazalishaji wa miche wameitaka serikali kufanya tathmini ya utunzaji wa miche inayogawiwa, pamoja na kutoa elimu juu ya matumizi salama ya mbolea kwa wakulima.