Mawaziri wa Afya kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamekutana jijini Arusha katika Mkutano wa 25 wa Kawaida wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Afya na kuridhia rasmi uanzishwaji wa Vituo viwili vya Umahiri vya Kikanda nchini Tanzania.
Uamuzi huo umetokana na mapendekezo yaliyowasilishwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu kuanzishwa kwa Kituo cha Umahiri cha Sayansi ya Afya ya Kinywa na meno kitakachokuwa chini ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na Kituo cha Umahiri cha Upandikizaji Uloto na Sayansi ya Magonjwa ya Damu kitakachokuwa chini ya Hospitali ya Benjamin Mkapa.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Mhe. Dkt. Godwin Mollel (Mb.) Naibu Waziri wa Afya na Kiongozi wa ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alieleza kuwa Tanzania itaendelea kuunga mkono ajenda ya afya ya EAC kwa kuimarisha mifumo ya afya, kuwekeza katika rasilimali watu na miundombinu ya afya ili kwenda sambamba na vipaumbele vya kitaifa na kikanda. Pia alisisitiza kuanzishwa kwa vituo vya umahiri ni hatua muhimu katika kuongeza uwezo wa huduma za afya maalum ndani ya kanda.
Katika kukabiliana na changamoto mpya za kiafya kama ugonjwa wa Mpox, Mhe. Dkt. Mollel alitoa wito kwa nchi wanachama kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa, kuboresha maabara, na kuongeza ushirikiano katika maeneo ya mipaka.
Vilevile alitoa msisitizo wa umuhimu wa ushirikishwaji wa jamii na mawasiliano sahihi katika kupambana na upotoshaji na unyanyapaa unaohusiana na magonjwa. Aidha, alisisitiza azma ya Tanzania kuendeleza elimu ya tiba kupitia miradi na program za kikanda na juhudi za kuoanisha mitaala ya tiba na udaktari katika Jumuiya.