Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali (mstaafu), Jacob Kingu amelipongeza Gereza la Songea kwa kuanza uzalishaji wa mkaa mbadala kwa ajili ya kupikia.
Mwenyekiti Kingu ametoa pongezi hizo leo wakati wa ziara yake katika Mkoa Ruvuma iliyolenga kutembelea na kukagua mifumo ya nishati safi ya kupikia katika Magereza iliyowezeshwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
“Kwanza niwapongeze kwa kuhama kutoka kwenye kutumia kuni na kuanza kutumia nishati safi ya kupikia. Lakini pia, niwapongeze kwa kuanza majaribio na kuanza rasmi kuzalisha mkaa mbadala unaotumika kama nishati safi ya kupikia.
Kwa kufanya hivyo, mtaweza kupunguza gharama ambazo mlikuwa mnatumia kununua makaa ya mawe kwa ajili ya kupikia na pia mtapata fedha baada ya kuuza mkaa huu mbadala katika taasisi nyingine na wananchi wanaotumia majiko banifu na hili litawawezesha kupata fedha mtazakazo wekeza katika miradi mingine ya kimaendeleo,” amesema Mwenyekiti Kingu.
Mwenyekiti huyo pia ameyataka magereza mengine kuiga mfano wa Gereza Songea kwa kuzalisha mkaa mbadala kwa ajili ya kupikia wao wenyewe kwa sababu rasilimali watu na malighafi zipo.
Ameahidi kuwezesha gereza hilo kupata mashine za kisasa za kuzalisha mkaa mbadala ili waweze kuzalisha mkaa bora zaidi na kwa wingi.
Kwa upande wake Mkuu wa Gereza la Songea, Robert Mabeja ameipongeza na kuishukuru REB pamoja na Uongozi wa REA kwa kuwapatia fedha kwa ajili ya kufunga mifumo ya nishati safi ya kupikia.
“Tangu tumeanza kutumia nishati safi ya kupikia tumeona mabadiliko makubwa sana. Chakula kinaiva kwa wakati na changamoto ya wafungwa kutoroka wakati wa kutafuta kuni tumeondokana nayo kabisa,” amebainisha Mkuu huyo wa Gereza.
Katika ziara yake hiyo ambayo alikuwa ameongozana pia na Mkurugenzi wa Umeme Vijijini kutoka REA, Mhandisi Jones Olotu, Kaimu Meneja wa Tanesco Mkoa wa Ruvuma pamoja na viongozi wengine wa Serikali, Mwenyekiti Kingu alitembelea pia Gereza la Kitai ambalo pia wanatumia nishati safi ya kupikia.