Na WAF – Songea, Ruvuma
Wananchi wa mkoa wa Ruvuma na Mikoa ya jirani ya Njombe, Lindi na Mtwara, wametakiwa kutumia Hospitali ya Peramiho ili kupata huduma mbalimbali za afya kwakuwa hospitali hiyo ina watalaamu na vifaa vya kutosha.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru Kitaifa Bw. Ismail Ali Uss ametoa wito huo leo Mei 10, 2025 wakati akifungua jengo la dharura (EMD) katika Hositali ya Rufaa ya Mtakatifu Joseph Peramiho, iliyopo katika wilaya ya Songea mkoani Ruvuma.
“Kwakweli Mwenge wa Uhuru wa Kitaifa umepita na kukagua katika hospitali yetu ya Rufaa ya Mtakatifu Joseph hapa Peramiho, mradi kwakweli umesimamiwa vizuri, mradi una ubora, wananchi mjitokeze kupata huduma katika hospitali hii ikiwemo wa mikoa jirani,” amesema Bw. Uss
Kwa upande wake Waziri wa Afya ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Peramiho Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na Sekta Binafsi inaendeea kushirikiana kwa kuwa ni washirika na sio washindani.
“Katika kuonesha ushirikiano huo, Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inalipa mishahara ya watumishi 295 kwenye hospitali hii ya misheni ya Mtakatifu Joseph hapa Peramiho,” amesema Waziri Mhagama.
Mwenge wa Uhuru upo mkoani Ruvuma leo ikiwa ni siku ya pili (2) ambapo unakimbizwa katika Halmashauri ya Songea vijijini na kesho utakimbizwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kwa lengo la kukagua, kufungua na kuweka jiwe la msingi katika miradi mbalimbali.