NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dkt. Mohamed Said Dimwa, akizungumza katika kongamano la kuwahamasisha Watu Wenye Ulemavu Zanzibar kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa Dola wa Oktoba 2025 lililofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul Wakil Unguja.
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dkt. Mohamed Said Dimwa,akiwa katika picha ya pamoja na viongozi na washiriki wa kongamano hilo.
BAADHI ya Washiriki wa Kongamano hilo wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi wa kongamano hilo ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dkt. Mohamed Said Dimwa.
………..
NA MWANDISHI WETU,ZANZIBAR.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dkt. Mohamed Said Dimwa, ametoa wito kwa watu wenye ulemavu nchini kuacha kuwa watazamaji na badala yake kuwa wahusika wakuu katika mchakato wa uchaguzi mkuu wa dola mwaka 2025.
Wito huo ameutoa katika kongamano la ushiriki wa watu wenye ulemavu kwenye uchaguzi mkuu wa 2025, lililofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil Unguja.
Dkt. Dimwa alisisitiza kuwa haki, usawa, na ushiriki wa kundi hilo ni ajenda ya kitaifa inayopewa kipaumbele na CCM.
Katika hotuba yake iliyojaa msisitizo na matumaini, Dkt. Dimwa alisema kuwa kwa mujibu wa Ibara ya 215 ya Ilani ya CCM ya mwaka 2020–2025, serikali kupitia chama hicho imeweka msingi imara wa kuwawezesha watu wenye ulemavu kwa vitendo.
Alitaja mafanikio yaliyopatikana ikiwa ni pamoja na utoaji wa ruzuku kwa zaidi ya jumuiya 40 za watu wenye ulemavu Zanzibar, kuundwa kwa mpango mkakati wa Baraza la Watu Wenye Ulemavu, na utekelezaji wa mpango kazi wa sera ya watu wenye ulemavu hatua ambazo zimechochea maendeleo jumuishi nchini.
“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeonyesha njia kwa kutekeleza maazimio haya kwa ufanisi mkubwa. Hiki ni kipindi cha matendo, si maneno,” alisisitiza Dkt. Dimwa huku akiwataka watu wenye ulemavu kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu za kugombea nafasi za udiwani, ubunge na uwakilishi kupitia CCM.
Dkt. Dimwa alisema angetamani kuona watu wenye ulemavu wakigombea nafasi mbalimbali katika majimbo bila kusubiri uteuzi, akisema CCM haina mwenye nacho, bali ni chama cha wote.
“Hakuna mtu mwenye hati miliki ya uongozi ndani ya CCM bali kila mtu mwenye sifa za kuwa raia wa Tanzania kwa mujibu wa sheria ana haki sawa ya kuongoza,” aliongeza kwa msisitizo.
Akizungumzia mustakabali wa CCM kuelekea uchaguzi wa Oktoba 2025, alieleza kuwa chama hicho kimejipanga kupata ushindi wa kihistoria kupitia utekelezaji wa ilani kwa vitendo, huku akivita vyama vya upinzani kuwa havina sifa,mvuto na ajenda za kuleta maendeleo nchini.
“Maendeleo haya si porojo, ni ushahidi wa kazi tunaposema barabara za kisasa,bandari za kisasa,viwanja vya ndege vya kisasa,skuli za ghorofa,mikopo na uwezeshaji kwa makundi yote,ujenzi wa masoko ya kisasa na mengine mengi wananchi wanayaona sio hadithi.
Dkt. Dimwa pia alitumia fursa hiyo kuwapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi kwa kusimamia vyema miradi mikubwa ya kimkakati inayolenga kufungua fursa za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni kwa watu wenye ulemavu.
Alisema chini ya uongozi wake, aliahidi kusimamia usawa na kupambana na vitendo vya rushwa ndani ya chama, ili kuhakikisha hadhi ya CCM inabaki kuwa imara na chama kinaendelea kuwa mikononi mwa wananchi wenyewe.
“Ni lazima tukirudishe chama mikononi mwa wananchi, kwa sababu wao ndio wamiliki halali wa CCM. Hatutakubali mfumo wowote wa upendeleo au rushwa kuhujumu mchakato wa kidemokrasia,” alisema kwa ujasiri.
Dkt.Dimwa aliwahakikishia watu wenye ulemavu nchini kuwa wanatakiwa kujiamini kwani wao ni sehemu ya maamuzi ya nchi si kwa hisani, bali kwa haki yao ya kikatiba.
Naye Mwakilishi wa Baraza la Wawakilishi kutoka kundi la watu wenye ulemavu, Mwantatu Mbaraka Khamis, alisema lengo la kongamano hilo ni kuwahamasisha watu wenye ulemavu kutoka makundi yote kushiriki katika uchaguzi na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Mwantumu,amezipongeza Serikali zote mbili kwa kuendelea kuweka mazingira bora kwa kundi hilo kupata haki na fursa zinazowajengea uwezo wa kijamii na kiuchumi.
“Tutaendelea kuwa mstari wa mbele kuunga mkono juhudi za serikali kupitia Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar (UWZ).
Tunataka Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ibaki kuwa nchi ya amani, mshikamano na maendeleo jumuishi,” alisema Mwantatu.
Mwakilishi huyo,alisema kuwa suala la usawa sio upendeleo, bali ni haki kwa watu wenye ulemavu, mwaka 2025 sio wa kusubiri bali ni wa kushiriki, kuongoza na kuamua hatma ya taifa.
Kongamano hilo lililoandaliwa na mwakilishi huyo kwa kushirikiana na Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar lilikuwa na mada mbalimbali za kuwajengea uwezo juu ya masuala ya kiuchumi,kijamii na kisiasa.