Naibu Mkuu wa Chuo Cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Dkt. Ephraim Mwasanguti akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi wa SACCOS Jijini Mwanza


Viongozi wa SACCOS kutoka mikoa ya Kanda ya ziwa wakiwa kwenye mafunzo
…………..
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imevitaka vyama vya ushirika wa akiba na mikopo (SACCOS) pamoja na taasisi nyingine zinazotoa mikopo nchini kuhakikisha zinatumia mfumo maalum wa kuhakiki taarifa za wakopaji kabla ya kutoa mikopo, ili kuepuka hasara zinazoweza kudhorotesha ustawi wa taasisi hizo.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatatu Mei 12, 2025 Jijini Mwanza na Naibu Mkuu wa Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania, Dkt. Ephraim Mwasanguti, wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi wa SACCOS kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa kuhusu matumizi ya Mfumo wa Taarifa za Mikopo Tanzania (Credit Information System), unaowasaidia kutambua historia ya wakopaji.
Alisema mfumo huo utazisaidia taasisi za fedha kujiendesha kwa faida na ufanisi mkubwa kutokana na mikopo chechefu kupungua.
“Pia itasaidia kujenga utamaduni wa kurudisha mikopo na kuongeza sifa za kuwa na kiwango kikubwa cha mkopo hatua itakayosaidia kukuza uchumi wa nchi”, Alisema Dkt. Mwasanguti
Kwa upande wake, Mrajis Msaidizi wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika wa Kifedha, CPA Josephat Kisamalala, amesema mfumo huo ni nyenzo muhimu kwa SACCOS katika kufanya maamuzi sahihi ya utoaji mikopo.
Naye Meneja masoko wa taasisi za fedha na vyama vya akiba na mikopo kutoka taasisi ya Credit Information, Emmanuel Matee aliishukuru BoT kwakuwapa leseni ya kupokea na kuchakata taarifa za mikopo
Baadhi ya wadau wa SACCOS walioshiriki mafunzo hayo wameeleza kuwa mfumo huo umekuwa msaada mkubwa katika kuwabaini wakopaji wasio na sifa, hivyo kuwasaidia kuepuka mikopo chechefu.