Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia,Profesa Adolf Mkenda,akiwasilisha bungeni Jijini Dodoma makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka 2025-2026.
Na Alex Sonna,Dodoma
KATIKA mwaka wa fedha 2025/26, Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imepanga kutekeleza vipaumbele vitano ikiwemo kuendelea na utekelezaji wa sera na mitaala, mapitio ya sheria na kuandaa
miongozo ya utoaji wa elimu na mafunzo.
Vipaumbele hivyo vimetajwa leo Mei 12,2025 bungeni na Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia,Profesa Adolf Mkenda wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025-2026.
Amevitaja vipaumbele vingine ni kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa mafunzo ya amali katika shule za sekondari na vyuo vya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.
Pia kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya awali, msingi, sekondari na
ualimu.
Vilevile kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya juu na kuimarisha uwezo wa nchi katika utafiti,
matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu ili kuchangia upatikanaji wa maendeleo endelevu.
“Katika hili, juhudi zaidi zitatumika kupeleka vijana wa Kitanzania kusomea mambo ya sayansi ya nyuklia, mambo ya kompyuta na akili-unde kwenye vyuo bora vilivyo nje ya nchi,”amesema Prof Mkenda