Mei 12, 2025, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda, aliwasilisha Bajeti ya Wizara yake ambapo aliomba kuidhinishiwa shilingi Trilioni 2.4, huku shilingi Trilioni 1.74 zikiwa ni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Moja ya taasisi muhimu chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ni Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB). Bodi hii inaratibu shughuli za kupokea maombi ya mikopo na kuwapangia mikopo waliokidhi vigezo vya mikopo. Aidha, Bodi inawajibika kukusanya mikopo kutoka kwa wanufaika wake hasa baaada ya kuhitimisha masomo yao na kuwa na vipato kupitia kuajiriwa au kujiajiri wenyewe.
Ndiyo maana, HESLB inatoa wito wa wanufaika wahitimu wenye vipato kujitokeza kwa hiari kulipa mikopo yao ili fedha hizo ziwanufaishe waombaji wengine ili kutengeneza idadi kubwa ya wanufaika kupitia fedha zinazorejeshwa kwa hiari.
Katika Bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026, idadi ya wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu inatarajiwa kuongezeka kutoka wanufaika 245,314 mwaka 2024/2025 hadi wanufaika 252,773 mwaka 2025/2026. Hii ni sawa na ongezeko la wanufaika 7,459.
Aidha, katika wanufaika 252,773 wanaotarajiwa kupata mikopo kwa mwaka ujao wa fedha 2025/2026, wanafunzi wa mwaka wa kwanza ni 88,320 huku wanafunzi wanaendelea wakiwa 164,453. Sanjari na hilo, wanafunzi 10,000 wa ngazi ya Stashahada (Diploma) wanaosoma programu za vipaumbele kama vile Sayansi Hisabati, Uhandisi na Teknolojia wanatarajiwa kunufaika na mikopo.
Bajeti ya Wizara ya Elimu kwa mwaka 2025/2026, haijasahau mwendelezo wa ufadhili wa Rais Samia (Samia Scholarships) kwa wanafunzi wenye ufaulu wa juu katika masomo ya sayansi. Katika ufadhili huo wa Rais Samia, wanafunzi 2,630 wanatarajiwa kunufaika, ambapo wanafunzi 1,220 ni wa mwaka wa kwanza, 80 ni wa Shahada za umahiri (Masters) na 1,330 ni wanafunzi wanaoendelea na masomo.
Pamoja na hayo yote, kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ukaguzi kwa waajiri 8,000 unatarajiwa kufanyika ili kufuatilia utii wa Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu. Kimsingi, Sheria ya Bodi ya Mikopo ya mwaka 2016 iliyofanyiwa marekebisho, sehemu ya 20 kifungu cha kwanza (1) inamtaka mwajiri kuwasilisha jina ya mtumishi mpya mwenye elimu ngazi ya Stashahada na kuendelea kwa Bodi ya Mikopo ndani ya siku 28 tangu alipoajiriwa ili kufahamu kama alinufaika na mikopo au la. Kushindwa kuwasilisha majina hayo kwa wakati, mwajiri atatozwa faini ya Shilingi 1,000,000 (Milioni Moja).
Vilevile, sheria hiyohiyo, sehemu ya 20 kifungu cha pili (2), inamtaka mwajiri kuwasilisha makato ya mshahara ya asilimia 15 ya mwezi ya mtumishi wake aliyebainika kuwa mnufaika wa mkopo isizidi Tarehe 15 ya mwezi unaofuata. Kushindwa kufanya hivyo, mwajiri atatozwa faini ya asilimia kumi ya fedha aliyopaswa kuiwasilisha.
Nihitimishe makala hii kwa kusisitiza kuwa kuguswa kwa HESLB kibajeti, kunaongeza fursa kwa vijana kupata elimu ya juu na hivyo kutimiza ndoto zao za kimaisha ambazo zina mchango mkubwa katika kuchochea maendeleo yao na ya nchi yetu kijamii, kiuchumi na kisiasa.
Dk. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Funguni ya wilayani Pangani mkoani Tanga.
Maoni: 0620 800 462.