Ameyasema hayo leo Mei 14, 2025 Jijini Dar es Salaam, Afisa Metrolojia Mwandamizi wa TBS Anectus Ndunguru wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea katika maadhimisho ya siku ya vipimo duniani yatakayofanyika Mei 20 mwaka huu ambapo kitaifa itafanyika mkoani Morogoro.
Aidha amesema kufanyika kwa uhakiki wa usahihi wa vipimo katika vifaa vya viwandani,usafiri wa anga, ujenzi na katika sekta mbalimbali utasaidia kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa viwandani kukidhi ubora,na kulinda usalama wa watumiaji pamoja na kutoa huduma bora.
Nduguru ameeleza kuwa vipimo vikihakikiwa kwa usahihi wake vitaleta manufaa kwa jamii katika nyanja mbalimbali za kiuchumi kwani watu watapata kitu kilicho bora katika kila sekta ikiwemo sekta ya Afya, ujenzi, Mawasiliano, Vyakula n.k kwa ajili ya ustawi na ubora wa bidhaa na huduma nchini.
Kwa upande wake Afisa Vipimo Mkuu wa TBS Joseph Mahila amesema kufanyika kwa huduma ya uhakiki wa vipimo mbalimbali katika shirika hilo kunawapunguzia kazi wahitaji kwani siku za nyuma walilazimika kwenda nje ya nchi kufuata huduma hiyo.
“Katika nchi za Afrika Mashariki nchi yetu kupitia maabara yetu imekuwa ya kwanza kupata ithibati katika eneo la torque,Barometa,na unyevu na kwa maana hiyo sasa TBS tumekuwa wa kwanza kutoa huduma ya ulinganifu wa vipimo katika ukanda wa Afrika Mashariki”Amesema.
Mbali na hayo Mahila amesema wanatarajia kupokea ugeni kwa nchi za Afrika Mashariki kwa ajili ya mafunzo ya eneo la torque,barometa, pamoja na vipimo vya unyevu.
Mei tano ya kila mwaka Tanzania inaungana na Mataifa Mengine Duniani kuazimisha siku ya vipimo ikiwa ni mwaka wa 150 tangu kuanzishwa kwake ambapo kwa mwaka huu imebeba kauli mbiu inayosema “Vipimo kwa nyakati zote na kwa watu wote”.