Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Same, Kilimanjaro – Mamia ya wakazi wa wilaya ya Same wamejitokeza kwa wingi katika Hospitali ya Wilaya ya Same kupata huduma za matibabu kutoka kwa madaktari bingwa waliotumwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan, chini ya kampeni ya kupeleka huduma za afya karibu na wananchi.
Huduma hizo za kibingwa zilianza kutolewa mwazoni mwa wiki hii na zimehusisha matibabu ya magonjwa mbalimbali yakiwemo ya wanawake, watoto, upasuaji, macho, na magonjwa ya ndani. Madaktari hao waliwasili mapema hospitalini hapo na kuanza kuhudumia wagonjwa kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo na mikoa jirani.
Akizungumza na Fullshangwe Media Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Same, Dkt. Alexander Alex, alisema ujio wa madaktari bingwa hao ni sehemu ya jitihada za serikali katika kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya bila kikwazo cha umbali wala gharama.
“Tunaishukuru serikali kwa kuwaleta madaktari hawa. Wananchi wengi hapa walikuwa wanapata shida kusafiri hadi Moshi au Dar es Salaam kwa ajili ya huduma hizi. Sasa matibabu haya yapo karibu nao, tena bila malipo makubwa,” alisema Dkt. Alex.
Baadhi ya wananchi waliohojiwa walieleza kufurahishwa na huduma hizo, wakisema ni faraja kubwa kwao kuona serikali inawajali kwa vitendo. “Nimepata huduma ya macho bure kabisa. Madaktari wametupokea vizuri sana,” alisema Bi. Zainabu Mussa mkazi wa Gonja.
Huduma hizo zitaendelea kwa muda wa siku kadhaa, huku hospitali hiyo ikishirikiana na viongozi wa jamii kuhakikisha kila anayehitaji matibabu anapata huduma ipasavyo.