Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imeendesha mafunzo maalumu kwa Wajasiriamali yenye lengo la kutoa elimu kwa wajasiliamali kuhusu usajili wa alama za biashara
Akiwasilisha mada Mei 13, 2025 katika Ofisi za SIDO, Jijini Dar es Salaam Afisa kutoka BRELA Athumani Makuka, amewahimiza wajasiriamali kutambua kuwa usajili wa Alama ya Biashara ni ulinzi halali na huongeza thamani ya biashara kwa kuongeza uaminifu wa wateja na utambulisho wa chapa yao sokoni. Alieleza kuwa alama ya biashara ni sehemu ya haki miliki (Intellectual Property) ambayo kila mjasiriamali anapaswa kuilinda kwa maslahi ya sasa na ya baadaye.
“Mafunzo hayo yamelenga kuwapa elimu wajasiriamali juu ya umuhimu wa kusajili Alama za Biashara na Huduma kama njia ya kulinda bidhaa na huduma zao kwenye soko lenye ushindani.”Amesema
Washiriki wa mafunzo hayo walionyesha ushirikiano wa hali ya juu kwa kuuliza maswali na kushiriki katika kuzungumzia uzoefu wao binafsi kuhusu changamoto za kufanya biashara bila usajili wa chapa. Wengi wao walikiri kuwa hawakuwahi kufahamu uzito wa haki miliki, lakini waliondoka kwenye mafunzo wakiwa na maarifa na hatua muhimu za kuchukua ili kusajili chapa zao kupitia BRELA.
Mafunzo hayo ni sehemu ya shughuli muhimu kuelekea maadhimisho ya Siku ya Miliki Bunifu Duniani (Intellectual Property Day) yatakayofanyika tarehe 21 Mei, 2025.
BRELA, imekua ikitoa mafunzo kwa wajasiriamali na wafanyabiashara kwa kutoa elimu juu ya umuhimu wa kulinda mali zao za kiakili ili kuendelea kuwapa fursa mbalimbali katika masoko.