KAMATI ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga wamefanya ziara maalumu ya ukaguzi wa uwanja wa CCM Mkwakwani ambao umefanyiwa maboresho makubwa na hivyo unaweza kutumika kwenye mchezo wa nusu fainali wa CRDB Federation Cup kati ya timu ya Yanga na JKT.
Akizungumza mara baada ya kuutembelea uwanja huo,Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga Rajab Abdurhaman alisema kwamba uwanja huo kutokana na maboresho makubwa upo tayari kwa ajili ya mchezo huo utacheza Mei 18 mwaka huu.
Alisema kwamba walifanya maboresho makubwa ya uwanja huo sehemu ya kuchezea ambayo ilikuwa na changamoto awali kwa jitihada walizifanya viongozi kwa kushirikiana na TFF kupitia Rais Karia waliwaunga mkono CCM kwa jitihada za kufanya ukarabati wa uwanja wao na TFF kugharamia majani sasa mambo yapo vizuri.
Aidha alisema lakini matarajio yao kwa kushirikiana na TFF wameshaandaa michoro namna ya kuubadilisha muonekano wa uwanja huo uwanja wa Mkwakwani kwa kuweka viti na kutengeneza jukwaa la kisasa.
“Lakini pamoja na hilo pia tutabadilisha muonekano wa vyumba vya kubadilisha nguo,vyoo nk na sasa hivi tumeshakamilisha michoro na tupo kwenye mchakato wa kutafuta wadau ili waweze kutuunga mkono
Hata hivyo alisema kwamba mchezo wa Nusu Fainali hiyo kuchezwa kwenye uwanja wa CCM Mkwakwani Jijini Tanga ni heshima kubwa kwao na wapo tayari kwa ajili ya mchezo huo.
Mwenyekiti huyo alitoa wito kwa wapenzi wa soka nchini kujitokeza kwa wingi kwenye mchezo huo ili kuweza kuipa sapoti nusu fainali hiyo .