Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mh. Adam Kigoma Malima, amesema ushirika ni nyenzo muhimu ya maendeleo katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa, na kwamba vyama vya ushirika vina mchango mkubwa katika kukuza pato la taifa kupitia shughuli za uzalishaji.
Akizungumza kwenye Jukwaa la Vyama vya Ushirika lililofanyika Mei 15, 2025, mkoani Morogoro, Mh. Malima alieleza kuwa sekta za kilimo, ufugaji, uvuvi, fedha na madini, zote zina nafasi kubwa katika kukuza maendeleo kupitia mfumo wa ushirika.
“Ninapenda kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mchango wake mkubwa katika kuviimarisha vyama vya ushirika nchini,” alisema Mh. Malima huku akihimiza wanachama wa ushirika kulipa kodi kwa hiari ili kuchangia maendeleo ya taifa.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa vyama vya ushirika kubadilika na kuingia kwenye mifumo ya kisasa ya kiutendaji kwa kutumia teknolojia na usimamizi wa kitaalamu, ili kuongeza ufanisi na tija kwa wanachama pamoja na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika Mkoa wa Morogoro, Bw. Idd Bilali, amesema kuwa vyama vya ushirika mkoani humo vimepata mafanikio makubwa kupitia matumizi ya TEHAMA, ambayo yameimarisha usimamizi wa vyama, kupunguza migogoro na ajali mashambani, na kurahisisha ukusanyaji wa kodi.
Hata hivyo, Bw. Bilali amesema licha ya mafanikio mbalimbali ambayo yamepatikana lakini bado kuna changamoto kadhaa zinazoathiri maendeleo ya vyama hivyo, ikiwemo ukosefu wa masoko ya uhakika kwa bidhaa, migogoro baina ya wakulima na wafugaji, pamoja na mzigo wa kodi usioendana na uwezo wa kifedha wa washirika.
“Tunaendelea kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali kutafuta suluhisho la changamoto hizi ili kuhakikisha vyama vya ushirika vinakuwa endelevu na vyenye tija,” alisema Bw. Bilali.
Jukwaa hilo lilihudhuriwa na viongozi wa serikali, wanachama wa vyama vya ushirika kutoka Wilaya za mkoa wa Morogoro, pamoja na wadau wa maendeleo ya ushirika.