Watumishi wa umma mkoani Mara wametakiwa kuzingatia kuwa suala la utoaji huduma bora kwa wananchi sio la hiari bali ni la lazima na kwamba yeyote atakayeshindwa kutimiza wajibu wake atachululiwa hatua za kisheria na kinidhamu.
Akizungumza wakati wa kupokea tuzo zilizotolewa na Ofisi ha Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Wizara ya Afya kwa vituo viwili vya kutolea huduma za afya katika Manispaa ya Musoma leo Alhamisi Mei 15,2025 Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi amesema suala la utoaji wa huduma bora na stahiki kwa wanachi ni jukumu la msingi kwa watumishi wote wa umma.
Kanali Mtambi amesema serikali imetoa fedha nyingi kuboresha miundombinu ya huduma mbalimbali za kijamii hivyo upatikanaji wa huduma bora katika miundombinu hiyo ni jambo ambalo linatakiwa kuzingatiwa.
“Kutakuwa hakuna maana kabisa kama tuna vituo bora vya kutolea huduma za kujamii lakini huduma zinazotolewa pale hazina viwango, nawaagiza watumishi wote wa umma wa kada zote kuhakikisha kila mtu kwa nafasi yake anatoa huduma bora inayokidhi viwango,” amesema
Amesema tuzo na vyeti vilivyotolewa kwa vituo hivyo viwili vya kutolea huduma za afya katika Manispaa ya Musoma vinapaswa kuwa chachu na morali kwa watumishi wote wa umma ili waweze kujituma na kutoa huduma inayokidhi mahitaji.
“Sisi ni watumishi wa wananchi,ni lazima tuwatumikie, tumeletwa hapa kila mmoja kwa nafasi yake kuwatumiakia wananchi hivyo suala la huduma bora ni la msingi zaidi, wananchi wanapaswa kupata huduma bora kama ambavyo serikali imekusudia, kila mmoja kwa nafasi yake anatakiwa kuiwezesha serikali kufanikisha lengo hilo,” amesema
Kufuatia vituo hivyo kupata tuzo hizo Kanali Mtambi amesema serikali ya mkoa itatoa jumla ya Sh2 milion kwa vituo vyote viwili kama motisha na kuwataka watumishi wa vituo hivyo kuongeza jitihada zaidi ili kuendelea kutoa huduma bora kwa jamii huku uongozi wa serikali wilayani Musoma ukitoa jumla ya Sh3 milioni kama motisha kwa wafanyakazi wa vituo hivyo.
Awali akitoa maelezo kuhusu tuzo hizo, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka amesema tuzo hizo zimetolewa na Tamisemi pamoja na Wizara ya Afya baada ya vituo hivyo kuibuka washindi kufuatia shindano lililoshirikisha vituo zaidi ya 3,700 nchini kuhusu utoaji wa huduma bora.
“Kituo cha afya Nyasho kimeibuka mshindi wa jumla kati ya vituo vya afya vilivyoshindanishwa huku zahanati ya Kwangwa ikiwa miongoni mwa zahanati 17 zinazotoa huduma bora nchini, sisi hii tunaitumia kama chachu kuhakikisha vituo vyote vinaboresha huduma ili wananchi waweze kufurahia uwekezaji unaofanywa na serikali katika sekta ya afya kwenye wilaya yetu,” amesema Chikoka
Wakizungumza baada ya kupokea tuzo na vyeti,waganga wafawaidhi wa vituo hivyo wamesema siri ya ushindi huo ni ushirikiano na kujituma kwa wafanyakazi katika vituo vyao ili kuhakikisha wanatoa huduma bora.
“Vigezo ni vingi vimetumika kuwapata washindi ila naamini ushirikiano wa wafanyajzi katika kituo chetu cha afya ili kuweza kutoa huduma stahiki kwa wateja wetu ndio siri kuu ya ushindi hivyo tunaahidi kuwa huduma zetu zitakuwa bora na zenye kukidhi viwango muda wote,” amesema Mganga mfawidhi wa kituo cha afya Nyasho Dk Richard Majahasi
Amesema licha ya kituo chake kuwa na idadi kubwa ya wateja ikiwepo wastani wa wajawazito 250 hadi 300 wanaojifungulia kituoni hapo kwa mwezi lakini wameweza kuhakikisha kila mgonjwa napata huduma bora na kwa wakati kwa mujibu wa mahitaji yake.
Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Kwangwa, Dk Christopher Bilia amesema tuzo hiyo inakwenda kuwa chachu na morali kwa wafanyakazi wa zahanati hiyo kuendelea lutoa huduma bora kwa wananchi.