Leo Mei 15, Waziri wa Madini Mhe.Anthony Mavunde, ameongoza watumishi wa wizara hiyo kuanza rasmi kazi katika jengo jipya la kisasa lililopo eneo la Mtumba, jijini Dodoma.
Uhamisho huo unamaanisha kuwa huduma zote za Wizara sasa zitapatikana katika eneo moja, hatua inayolenga kuondoa usumbufu uliokuwa ukiwakumba wananchi waliolazimika kufuata huduma katika maeneo tofauti .
Akizungumza Mei 15,2025 kwenye Ofisi za Wizara hiyo wakati wa kuwasili kwa mara ya kwanza katika jengo hilo, Waziri Mavunde amesema kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini lililotaka wizara hiyo kuhamia katika Ofisi hiyo .
Ameongeza kuwa amekamilisha ahadi yake ya kuhakikisha wizara hiyo inahamia rasmi kama sehemu ya mageuzi ya kiutendaji.
Waziri huyo ameeleza kuwa kukamilika kwa jengo hilo ni matokeo ya usimamizi mzuri na mshikamano wa watumishi wa wizara na kuwapongeza kwa kazi kubwa waliyoifanya kuhakikisha mradi huo wa unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.
Amesema kuwa hatua hiyo ni ushahidi wa namna Serikali ilivyojipanga kuboresha huduma kwa wananchi.
“Tunataka wananchi wapate huduma kwa urahisi bila kukimbizana kutoka ofisi moja hadi nyingine,kwa sasa, vitengo vyote muhimu vya wizara vinapatikana hapa Mtumba,hii ni hatua kubwa ya kuimarisha utendaji wetu,” amesema Mavunde.
Mbali na kuwahakikishia wananchi huduma bora, Waziri Mavunde ameeleza kuwa wafanyabiashara waliopo katika sekta ya madini nao watanufaika na uboreshaji wa miundombinu hiyo.
Amesema mazingira bora ya kazi yanayopatikana Mtumba yataongeza ufanisi katika utoaji wa leseni, usimamizi wa shughuli za uchimbaji na ufuatiliaji wa sekta kwa ujumla.
Waziri Mavunde amewataka watumishi wote wa Wizara ya Madini kuendelea kuwa weledi na wawajibikaji katika kuhudumia wananchi, akisema kuwa jengo jipya ni fursa mpya ya kuonyesha mabadiliko katika utoaji wa huduma bora kwa taifa.