Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo(Mb.), amesisitiza dhamira ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na Jamhuri ya Finland kwa manufaa ya pande zote.
Msimamo huo ameutoa jijini Dar es Salaam alipozungumza katika Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Finland, lililowakutanisha wadau mbalimbali kutoka sekta za umma na binafsi za Tanzania na Finland.
Mhe. Kombo amewahakikishia wawekezaji kutoka Finland kuwa Tanzania imeendelea kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini na kuongeza kuwa maboresho hayo yanalenga kurahisisha utoaji wa leseni, kupunguza urasimu na kuboresha mifumo ya forodha ili kuongeza ufanisi wa huduma kwa wawekezaji.
Amebainisha kuwa Serikali iko tayari kushirikiana na kuhudumia wawekezaji kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
Waziri Kombo ametaja teknolojia ya habari na mawasiliano, afya, dawa, na teknolojia za kilimo kuwa ni miongoni mwa sekta zenye fursa kubwa za uwekezaji na ushirikiano.
Amesema Tanzania haitaki kuwa soko tu la bidhaa kutoka Finland, bali inataka kuwa mshirika wa muda mrefu na wa kuaminika katika biashara na uwekezaji.
Aidha, amewahimiza wafanyabiashara wa Kitanzania kuchangamkia fursa zilizopo katika soko la Finland na kubainisha kuwa Finland inathamini ubora, uendelevu na uwazi ambapo bidhaa za asili kutoka Tanzania zina uwezo wa kuvifikia na hivyo kuimarisha biashara kati ya nchi hizo.
Naye Rais wa Jamhuri ya Finland, Mheshimiwa Alexander Stubb, amepongeza jitihada za Tanzania za kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuelezea kuwa Finland iko tayari kushirikiana bega kwa bega na Tanzania katika maeneo ya Elimu na Ufundi, nishati, afya, kilimo na mazingira kwa manufaa ya pamoja.
Mheshimiwa Rais Stubb amesisitiza kuwa Finland inaiona Tanzania kama lango muhimu kuelekea masoko ya Afrika Mashariki.
Rais wa Finland yupo nchini kwa ziara ya kitaifa na ameambatana na ujumbe wa wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Finland.