Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Upngosll, Kadari Singo, akizungumza katika hafla ya mahafali ya taasisi ya Uongozi Institute yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City jijin.
Mke wa Rais wa Finland, Suzanne Innes-Stubb akizungumza katika mahafali hayo yaliyofanyika ukumbi wa Malimani City jijini Dar es salaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene akifafanua Mambo kadhaa katika hafla Hi you.
……………….
Taasisi ya Uongozi imehitimisha mahafali yake ya nane kwa mafanikio makubwa, ambapo zaidi ya viongozi 200 kutoka sekta mbalimbali wamehitimu mafunzo ya muda mrefu ya uongozi, ikiwa ni hatua muhimu katika kukuza kizazi cha viongozi wenye maono, weledi, na uadilifu barani Afrika.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika leo Mei 16, 2025 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Kadari Singo, alisema kuwa wahitimu wamekamilisha programu tatu kuu: Stashahada ya Uzamili ya Uongozi (PGD), Cheti cha Uongozi (CiL), na Mpango wa Uongozi kwa Wanawake (WLP). Alieleza kuwa programu hizo zimewahusisha viongozi kutoka serikali, sekta binafsi, vyuo vikuu na asasi za kiraia kutoka nchi mbalimbali za Afrika.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Mke wa Rais wa Finland, Suzanne Innes-Stubb, alisisitiza umuhimu wa viongozi kufanya maamuzi kwa kuzingatia ukweli na si kwa hisia au dhana, hasa katika enzi hii ya taarifa potofu na upotoshaji. “Ni lazima viongozi watambue kuwa maamuzi yao yana athari kubwa kwa wananchi; hivyo, ukweli na maadili viwe nguzo kuu,” alisema.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, alisisitiza umuhimu wa kufanya maboresho katika mchakato wa uthibitishaji wa wakurugenzi wakuu ili kuepusha migogoro kazini, huku akihimiza matumizi bora ya rasilimali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Washirika wa maendeleo nao walieleza dhamira yao ya kuendelea kusaidia juhudi za kukuza uongozi bora nchini. Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Christine Grau, alisisitiza kuwa “uongozi bora hujengwa na timu zenye utofauti wa mawazo,” huku akihimiza kujitolea kwa dhati kwa ajili ya maendeleo ya taifa.
Mkuu wa Ushirikiano wa Ubalozi wa Finland nchini Tanzania, Juhana Lehtinen, aliitaja Taasisi ya Uongozi kuwa ni ishara ya ushirikiano wa muda mrefu kati ya Finland na Tanzania, akisisitiza kuwa serikali yake itaendelea kuunga mkono jitihada za taasisi hiyo.
Aidha, Katibu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed Said, aliwahimiza wahitimu kutumia ujuzi walioupata kuhamasisha wengine na kuchangia maendeleo yenye maana kwa jamii.
Taasisi ya Uongozi imejikita katika kukuza viongozi wa sasa na wa baadaye, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kujenga utawala bora, uwajibikaji, na maendeleo endelevu ya Tanzania na kanda nzima ya Afrika.