Na Sophia Kingimali.Dar es salaam.
UONGOZI wa Chuo Cha Uuguzi Mchukwi kutoka wilayani Kibiti mkoani Pwani, kimefungua tawi jipya katika Chuo cha Ufundi Furahika(VETA)lengo likiwa kuendelea kutoa elimu ya Afya kwa vijana ili kuongeza idadi ya watoa huduma za afya katika hospitali zilizopo nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo May 16,2025 Jijini Dar es sala Mkuu wa Chuo cha Uuguzi Mchukwi, Malsel Daniel, baada ya kusaini makubaliano ya kuanzisha tawi hilo katika Chuo Cha Furahika, amesema wamekusudia kusogeza huduma hiyo jijini Dar es Salaam ili kwa wahitaji wapate fursa ya kusoma wakiwa karibu na maeneo yao.
Pia ameongeza kuwa sababu nyingine ambayo imewasukuma kufungua tawi lao hapo ni namna uongozi wa Chuo Cha Furahika ulivyotoa ushirikiano wa karibu tangu mchakato ulivyoanza hadi kufikia kusaini makubaliano hayo ambayo dhahiri yatakuwa na tija stahiki.
“Tofauti na hayo, sababu nyingine ya kufungua tawi ndani ya Chuo Cha Furahika, mradi huu utasaidia kusukuma mbele agenda ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Watanzania wanapata huduma ya afya popote walipo,” amesema.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mchukwi, Dkt Japhet Guzuye amesema maono yaliyosababisha kuanzishwa Chuo Cha Uuguzi, Mchukwi kilichopo wilayani Kibiti, mkoani Pwani, pia yamechochea kufungua tawi katika Chuo Cha Furahika jijini Dar es Salaam, hivyo kwao ni furahika kufikisha huduma hiyo katika eneo hilo.
“Kwakweli kwetu ni furaha kufungua tawi hapa kwani maono tuliyoanza nayo kufungua Chuo Cha Mchukwi, tutayaendeleza hapa ambayo tunaamini yatasaidia kuongeza wahudumu katika sekta ya afya hapa nchini, amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo Cha Ufundi Furahika VETA,Dkt David Msuya amesema chuo tayar kimejipanga na kipo tayari kutoa mafunzo kwani wanamadarasa ya kutosha na vitendea kazi hivyo chuo kipo tayari kutoa mafunzo hayo kulingana na vigezo vilivyowekwa na mamlaka.
“Kwa kuwa ndoto yetu imetimia nawaomba wazazi kuwaleta watoto wao hapa kwaajili ya kupata mafunzo ya uuguzi na ukunga, pia waingie katika mtandao wa Chuo cha Mchukwi ili waweze kuomba nafasi ya kujiunga na tawi la hapa na tayari dirisha la usahili limefunguliwa”.
Pia niushukuru uongozi wa Chuo Cha Mchukwi kwa kukamilisha jambo hili ambalo limakuja kutimiza ndoto za vijana wetu, pia niishukuru Serikali yetu chini ya Rais Dkt Samia kwa kuendelea kutuunga mkono katika jitihada hizi za kutoa elimu bure kwa jamii yenye uhitaji,” amesema.